News

Utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Barabara ya lami Tanga hadi Pangani wafikia asilimia 74

Utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Barabara ya lami Tanga hadi Panganiwafikia asilimia 74

 

Bagamoyo

13 April, 2024

Utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara ya Bagamoyo (Makurunge) - Saadani - Pangani - Tanga (km 256); sehemu ya kwanza Tanga Mjini hadi Pangani km 50 umefikia asilimia 74.

Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni; Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Tanga Mha. Dastan Singano amesema mradi huo unatarajiwa kukamilika Disemba mwaka huu 2024.

Mha. Singano amesema ujenzi wa barabara hiyo ya kiwango cha lami ambao kwa sehemu kubwa unapita katika Wilaya ya Pangani; sehemu ya kwanza Tanga – Pangani unatekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 70 ambazo ni fedha za ndani kutoka Serikalini.

Ameeleza “Tunamshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kweli ndio aliyewezesha kupatikana kwa fedha nyingi kiasi hiki kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hii kwa hiyo hii miradi itakapokamilika pamoja na faida nyingine nyingi lakini itapunguza muda wa safari, watu watasafiri muda mfupi na kwa starehe zaidi’’.

Aidha mradi wa ujenzi wa barabara ya Bagamoyo (Makurunge) - Saadani - Pangani - Tanga (km 256) unaounganisha Mikoa ya Tanga na Pwani kupitia Bagamoyo; ukikamilika utafungua fursa za kiuchumi, usafiri na usafirishaji katika mwambao wa Tanga, Mikoa ya jirani pamoja na Nchi Jirani ya Kenya.