RAIS SAMIA ASIKIA SAUTI YA WANANCHI WA DAREDA- MANYARA
Manyara
06 Aprili, 2024
Serikali kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imesaini mkataba wa ujenzi barabara ya Dareda- Dongobesh (Km 60) sehemu ya Dareda Centre - Dareda Mission (Km 7.0) kwa kiwango cha lami lengo ni kuendelea kuongeza mtandao wa barabara za lami nchini na kuinua uchumi wa wananchi kupitia sekta ya ujenzi.
Akizungumza kwenye hafla iliyofanyika leo tarehe 6 Aprili 2024 katika eneo la mradi mkoani Manyara; Waziri wa Ujenzi Mhe. Innocent Bashungwa amesema sehemu hiyo ya barabara inagharamiwa kwa fedha za ndani kwa asilimia 100 na itakapokamilika itasaidia kuondoa adha ya usafiri na usafirishaji wa mazao ya kilimo, mifugi na misitu katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Manyara.
Amesema Serikali ina mpango wa kutekeleza miradi mitatu mikubwa katika mkoa wa Manyara ikiwa ni pamoja na ile kushirikisha wabia kwa utaratibu wa EPC+ Financing; ambapo takribani kilomita 515 za barabara za kiwango cha lami zitajengwa katika mkoa huo.
Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mha. Mohamed Besta, amesema barabara hiyo itajengwa kwa kuzingatia matakwa ya kimkataba na kwa mujibu wa usanifu ambao utasimamiwa na wataalamu wa ndani kutoka Kitengo cha Usimamizi wa Miradi cha TANROADS (TECU).
Amesema utekelezaji wa mradi wa ujenzi barabara hiyo ya Dareda - Dongobesh (Km 60) umegawanyika katika sehemu mbili, sehemu ya kwanza ni kutoka Dareda Centre - Dareda Mission (Km 7) na sehemu ya pili ni kutoka Dareda Mission- Dongobesh (Km 53).
Mha. Besta ametoa wito kwa Mkandarasi anayejenga barabara hiyo Kampuni ya M/s Jiangxi Geo Engineering (Group) Corporation ya nchini China, kufanya kazi kwa weledi wa hali ya juu ili kazi zote zikamilike ndani ya muda uliopangwa kwa kuzingatia viwango na gharama zinazokubalika.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga, amesema kukamilika kwa barabara hiyo kutafungua fursa za kiuchumi kwa Wananchi wa Babati vijijini na Mbulu, kwani wataweza kusafirisha mazao yao kwa urahisi zaidi huku akiipongeza TANROADS kwa kufanya kazi nzuri.