TANROADS YACHUKUA HATUA ZA HARAKA KUHAKIKISHA BARABARA KUU WA LINDI-PWANI-DAR ES SALAAM INAPITIKA WAKATI WOTE
Lindi
05 April, 2024
Serikali kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kukabiliana na athari za mafuriko ya maji ya mvua za El- nino zinazoendelea kunyesha Mkoani Lindi ikiwa ni pamoja na kujenga njia ya mchepuo katika eneo la Mbwemkuru katika Barabara kuu ya Lindi hadi Dar- es Salaam, Kilomita 70 kutoka Lindi Mjini.
Pia imeendelea kufanya ukarabati wa kuhakikisha barabara inapitika wakati wote katika maeneo mengine korofi yaliyopo katika barabara hiyo ya Njia nne au njia panda kilomita 200 na eneo la Somanga kilomita 220 kutoka Lindi Mjini.
Meneja wa TANROADS Mkoa wa Lindi Mha. Emil Zengo amesema hayo tarehe 5 Aprili 2024 alipofanya ukaguzi wa maeneo mbalimbali yaliyoathiriwa na mvua hizo ambapo amesema timu ya Watalaam wa TANROADS na Wakandarasi wapo kwenye maeneo hayo wakiendelea na kazi mbalimbali za matengenezo kuhakikisha wanarejesha miundombinu yote iliyoharibiwa.
“Baada ya kufanya tathmini ya kihandisi tumeona eneo hilo la Mbwemkuru magari bado yanaweza kuendelea kupita upande mmoja lakini maji bado yanaendelea kuja, kwenye Mto huu hata mvua zisiponyesha maeneo ya hapa karibu maji yanakuja, tulichoamua ni kutengeneza barabara ya mchepuko ili chochote kitakachotokea mawasilianio ya barabara yasikatike na magari yaendelee kupita katika barabara hiyo ya mchepuko ambayo pia itatumika wakati wa ukarabati wa Kalvati lililoharibiwa’’. Amesema.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Lindi Mhe. Shaibu Ndemanga amesema “leo ni siku ya nne tupo hapa kalvati maarufu kama namba moja ukiwa unaelekea Lindi kutoka Dar- es Salaam limetitia upande mmoja, wenzetu wa TANROADS wamehamia hapa, wanalala hapa, wanamkia hapa wakiendelea na kazi kuhakikisha kwamba magari yanapita wakati wote huku wakiendelea na marekebisho’’.
“Nawapongeza sana TANROADS kuna kazi inafanyika hapa kuhakikisha wanajaza mawe pembeni ya barabara ambapo maji yanapita angalau kuzuia maji kuendelea kusababisha mmomonyoko wa barabara pamoja na kujenga njia ya mchepuo ili ikitokea kalvati limekatika basi magari yaendelee kupita’’. amesema.