News

SERIKALI YA AWAMU YA SITA YAKAMILISHA UKARABATI WA UWANJA WA NDEGE WA MTWARA NA BARABARA YA LAMI KM 50 KUTOKA MTWARA HADI MNIVATA

SERIKALI YA AWAMU YA SITA YAKAMILISHA UKARABATI WA UWANJA WA NDEGE WA MTWARA NA BARABARA YA LAMI KM 50 KUTOKA MTWARA HADI MNIVATA

Mtwara

03 April, 2024

SERIKALI kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imekamilisha ukarabati wa kiwanja cha Ndege Mtwara pamoja na ujenzi wa kilomita 50 za kiwango cha lami kutoka Mtwara hadi Mnivata katika barabara ya Mtwara – Tandahimba – Newala hadi Masasi.

 

Hayo yamesemwa na Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mkoa wa Mtwara Mhandisi. Dotto John Chacha alipozungumza na waandishi wa Habari kuhusu mafanikio ya miaka mitatu ya Serikali ya awamu ya sita chini Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

 

Amesema maboresho katika kiwanja hicho cha Ndege yamegharimu shilingi bilioni 57 zikihusisha ujenzi wa njia ya kuruka na kutua ndege na uwekaji wa miundombinu mingine ikiwemo ya taa ambayo inawezesha ndege kubwa na ndogo kutua na kuruka kiwanjani hapo masaa 24.

 

Amesema ujenzi wa barabara ya Mtwara – Tandahimba – Newala hadi Masasi km 210 inayopita katika majimbo saba umegawanywa katika awamu tatu; awamu ya kwanza ni kuanzia Mtwara - Mnivata Km. 50, ujenzi umeshakamilika kwa gharama ya shilingi bilioni 103; awamu ya pili kilomita 160 zilizobaki Serikali imeweka Wakandarasi wawili, mmoja akianzia Mnivata hadi Mitesa km 100 kwa gharama ya shilingi bilioni 142 na sehemu ya tatu km 60 gharama ya ujenzi ni shilingi bilioni 92 ikihusisha ujenzi wa daraja la Mwiti, sehemu zote Wakandarasi wapo maeneo ya mradi wakiendelea na kazi ya ujenzi.

 

Amesema ujenzi wa daraja kubwa la Mbangala lenye urefu wa mita 120 katika barabara ya ulinzi nao unaendelea kwa gharama ya shilingi bilioni 9.2.

 

Ameeleza kutokana na kutumika muda mrefu na kuchakaa, Serikali imepanga kukarabati upya na kwa kisasa zaidi barabara ya Mtwara – Mingoyo – Masasi km 200, ambapo itaweka Wakandarasi wawili ili kuharakisha ujenzi (Mradi upo hatua ya manunuzi).

 

Mha. Chacha amesema barabara nyingine ni Masasi – Nachingwea hadi Liwale km 175 ambayo itatekelezwa kwa utaratibu wa EPC + F mkataba ulishasaini muda wowote Mkandarasi ataanza kazi na kwamba hivi karibuni Serikali itatangaza zabuni ya ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami inayoanzia Mangamba – Madimba hadi Msimbati na Madimba – Tangazo hadi Kilambo.

 

Amesema hata hivyo Serikali kupitia TANROADS imekusudia kufanya usanifu barabara za Mtama hadi Newala na barabara ya Mbuyuni – Makongonda hadi Newala ili ziweze kujengwa kwa kiwango cha lami.