MIRADI 6 YA KIMKAKATI KUFUNGUA JIJI LA DODOMA
Dodoma
01 April, 2024
Kutokana na Ongezeko na kukuwa kwa kasi kwa jiji la Dodoma, Serikali ya Awamu ya Sita inaenda kufungua jiji hilo kwa kutekeleza Miradi ya Ujenzi wa Miundombinu ya Barabara, Madaraja na Kiwanja cha ndege.
Hayo yamesemwa na Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mkoa wa Dodoma Mhandisi Zuhura Amani, alipokuwa akizungumza na waandishi wa Habari kuhusu Mafanikio ya miaka mitatu ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hasan Madarakani.
Miradi hiyo sita ni pamoja na Ujenzi wa Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Msalato, Ujenzi wa Barabara ya mzunguko wa nje wa jiji la Dodoma, Barabara ya Ntyuka - Mvumi - Kikombo (km 76), Barabara ya Kongwa-Mpwapwa ambayo inajengwa kwa Awamu mbili, Barabara ya Mpwapwa - Ving’awe pamoja na ujenzi wa madaraja manne (4).
“Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ndani ya Miaka mitatu ya uongozi wake kwa kuweza kutekeleza zaidi ya miradi 6 katika jiji letu la Dodoma, na itakapokamilika itaongeza chachu ya kiuchumi na kijamii mkoani humu” amesema Mha. Zuhura
Mha Zuhura, ameongeza kwa kusema kuwa Usanifu wa barabara ya mzunguko wa Kati wa jiji la Dodoma (Km 47), ambapo km 23 umekamilika ni barabara ya Nanenane - Miyuji - Mkonze hadi Ntyuka, Utanuzi wa Njia nne Morogoro - Dodoma (Km 263) pamoja na Barabara ya Mpwapwa - Gulwe - Chipogoro (Km 75.4)
Vilevile, amesema katika miradi hiyo Serikali imewawezesha zaidi ya watanzania 1560 katika jiji la Dodoma kupata ajira kwenye miradi ambayo inaendelea kutekelezwa, na wameweza kufunga takribani taa 620 na kupanda miti 2652.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya matengenezo TANROADS - Dodoma, Mha. Elsony Mwekadzi amesema wanaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita, ndani ya Miaka mitatu wamefanikiwa kufanya ukarabati wa matengenezo katika barabara za jiji la Dodoma.
Vilevile, amesema Miradi yote ya matengenezo ya barabara na ukarabati wa madaraja umetekelezwa na wakandarasi wazawa ili kuwajengea uwezo katika kufanya kazi kubwa na ndogo.
Mkoa wa Dodoma unahudumia mtandao wa barabara wenye jumla ya kilometa 1,707.22, ukiwa na madaraja 332 kati ya hayo 155 yapo katika barabara kuu na 177 yapo barabara za Mkoa.