TANROADS yawahakikishia usalama watumiaji wa barabara ya Nyerere hadi Gongolamboto
Dar es Salaam
31 Machi, 2024
Serikali kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imeweka mazingira mazuri kwa watembea kwa miguu kwenye barabara ya mabasi ya Yaendayo Haraka (BRT - 3) Nyerere hadi Gongolamboto Jijini Dar - es Salaam.
Akizungumza hivi karibuni Msimamizi wa mradi huo Mha. Frank Mbilinyi amesema Wananchi waendao kwa miguu wanaotumia barabara hiyo, watalindwa kwa kuwekewa, alama za pundamilia, vivuko maalumu na taa za kuwaruhusu kuvuka kila wanapovuka upande mmoja kwenda mwingine na kutawekwa matuta kwenye barabara ya lami ya kawaida ili kupunguza mwendokasi wa magari.
“Kama mnavyoona kuna taa za kuvukia watu kwenye eneo la kuvukia Wananchi hata katika kila barabara za kawaida na zile zenye miundombinu ya mwendokasi kwa kuwasaidia kufika vema wanapokwenda kwenye vituo vya mabasi hayo au kuvuka kutoka upande mmoja na kwenda mwingine, hivyo hawataweza kupata madhara aidha kugongwa na magari au pikipiki, pia kutajengwa vivuko maalum vya wao kupita wanapokwenda kuepusha madhara,” amesema.
Amesema ujenzi huo wa barabara ya Mabasi Yaendayo Haraka ( BRT 3) unaotarajiwa kukamilika Machi 2025 umefikia asilimia 45 kwa Mkandarasi kuanza kujengea nguzo za vituo vya mabasi, pia kumwagia maji mara kwa mara, ili kuondoa vumbi lisilete madhara kwa watumiaji wa barabara ambayo ujenzi unaendelea.
Mha. Mbilinyi amesema barabara za Mabasi Yaendayo Haraka zimeshaanza kujengwa kwa matabaka mbalimbali yakiwemo tabaka la zege kuziruhusu kupitika kwa urahisi.
Aidha amewaasa watumiaji wa barabara hiyo wenye vyombo vya moto kuhakikisha wanafuata sheria za barabarani ili kuepuka kusababisha msongamano usio wa lazima.