News

SERIKALI YA AWAMU YA SITA YAENDELEA KUUFUNGUA MKOA WA KIGOMA KWA BARABARA ZA LAMI  

SERIKALI YA AWAMU YA SITA YAENDELEA KUUFUNGUA MKOA WA KIGOMA KWA BARABARA ZA LAMI

 

Kigoma

28 Machi, 2024

Serikali ya Awamu ya sita inayoongozwana Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inatekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo Mkoani Kigoma ikiwemo ujenzi wa barabara za lami njia nne Kigoma - Kidahwe na Kigoma - Ujiji lengo ni kuufungua Mkoa huo kiuchumi.

Hayo yamesemwa na Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mkoa wa Kigoma Mha. Narsis Choma, alipozungumza na waandishi wa Habari kuhusu Mafanikio ya miaka mitatu ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan madarakani.

"Katika kipindi hiki cha miaka mitatu ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Serikali yetu imeweza kutekeleza ujenzi wa njia nne katika mkoa wetu wa Kigoma na ukikamilika ujenzi huu utasaidia sana wananchi wa mkoa huu kiuchumi na kijamii kwani utarahisisha usafiri na usafirishaji” amesema Mha. Choma

Amesema ujenzi wa miradi hiyo unatokana na Mkoa huo kuwa na ongezeko la watu na barabara kuwa ndogo huku wafanyabiashara wengi wanaosafirisha mizigo yao kwenda nchi za jirani wakiendelea kupitia mkoani Kigoma.

Amesema pia katika kipindi cha miaka mitatu Serikali imetoa fedha za ujenzi wa barabara ya kutoka Uvinza hadi Malagarasi yenye urefu wa km 51.1, barabara ya Chagu (Kigoma) hadi Kazilambwa Tabora yenye urefu wa 36Km.

Pia kuna utekelezaji wa ujenzi kwa kiwango cha lami; Barabara ya Kibondo-Mabamba hadi Mpakani mwa Tanzania na Burundi (Mkarazi) yenye urefu wa km 47.7
na Barabara ya Mapandanjia ya Nduta (Malolegwa) hadi Kibondo Mjini.

Mha. Choma amesema katika kipindi hicho Mkoa wa Kigoma umefungwa taa za barabarani katika maeneo ya mjini pamoja na runinga za kutangaza miradi na kazi zinazofanywa na Wakala huo; na kwamba kupitia miradi yote ya matengenezo, Serikali imeweza kuwajali wakandarasi wa ndani kwa kuwapa miradi mikubwa ya kusimamia ili kuwajengea uwezo zaidi.

Naye Kaimu Meneja wa Idara ya Matengenezo wa TANROADS - Kigoma, Mha. Damian Kulaya, amesema wanaamshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuleta fedha kiasi cha shilingi bilioni 55.8 kwa ajili ya kufanya matengenezo ya barabara za lami na changarawe.