News

Rais Samia afanya mageuzi makubwa ya miundombinu mkoa wa Katavi

Rais Samia afanya mageuzi makubwa ya miundombinu mkoa wa Katavi

Katavi

24 Machi, 2024

Katika kipindi cha miaka mitatu cha Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan madarakani, Serikali ya awamu ya sita imefanya mageuzi makubwa ya ujenzi wa miundombinu ya barabara na madaraja mkoani Katavi.

Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Katavi Mhandisi Martin Mwakabende ametoa kauli hiyo wakati alipozungumza na waandishi wa Habari kuhusu mafanikio ya miaka mitatu ya Serikali ya awamu ya sita katika ujenzi wa miundombinu ya barabara na madaraja.

“Tunampongeza kwa dhati Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kukamilisha ujenzi kwa kiwango cha lami barabara ya Mpanda-Tabora (km 337.429), sehemu ya pili ni Komanga-Kasinde ( Km 108), pamoja na barabara ya Kasinde-Mpanda (Km 105.389) ndani ya miaka mitatu” amesema Mha. Mwakabende.

Mha. Mwakabende amesema, miradi mingine ya kimkakati na ya kitaifa inayoendelea kutekelezwa mkoani hapo ni pamoja na barabara ya Mpanda-Uvinza-Kanyani (km 250.44), Kibaoni- Sitalike, sehemu ya Kibaoni-makutano ya Mlele (km50), barabara ya Kagwira-Karema (km 110.29), ujenzi wa kitanda cha Daraja la Kavuu (urefu wa mita 87.5)

Pia miradi mingine ni ujenzi wa daraja jipya la Mirumba (mita 60), daraja jipya la Mto Lugufu (mita 42), ambalo kukamilika kwake kutatua changamoto ya muda mrefu ya wakazi wa Mishamo na Lukoma.

“ Miradi hii itakapokamilika itasaidia sana Wananchi wa Katavi kwani itarahisisha usafiri na usafirishaji wa kutoka Katavi kwenda Kigoma, Mbeya na mikoa mingine kwa haraka zaidi kwani Serikali inaenda kufungua mkoa wa Katavi kwa miundombinu ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami.” Ameeleza Mha. Mwakabende.

Amesema katika kipindi hicho wamefanikiwa kufunga jumla ya taa 719 kwenye barabara mbalimbali zikiwa ni sawa na asilimia 77.15 , na kufanya mkoa huo uwe na jumla ya taa 932 zenye thamani ya Shilingi Bilioni 2.

Pia, ametoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Katavi kulinda miundombinu ya barabara pamoja na kuacha kufanya shughuli za kibinadamu kwenye hifadhi ya barabara kwani kufanya hivyo kutasababisha zishindwe kudumu kwa muda mrefu zaidi.

Kwa upande wake Mkuu wa kitengo cha Miradi ya Maendeleo kutoka TANROADS Katavi, Mhandisi Albert Laizer amesema wanaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kuwaletea fedha za kufanya matengenezo ya barabara.