News

Serikali kuifungua Songwe kwa miradi 9 ya kimkakati ya barabara na madaraja

Serikali kuifungua Songwe kwa miradi 9 ya kimkakati ya barabara na madaraja

 

Songwe

19 Machi, 2024

Serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imekusudia kutekeleza miradi mikubwa tisa (9) ya kimkakati  ikiwemo upanuzi wa barabara kuu ya TANZAM kipande cha Igawa – Tunduma (km 218) na Ujenzi wa kituo cha ukaguzi wa pamoja wa magari katika barabara hiyo eneo la Iboya Mkoani Songwe.

 

Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Songwe Mhandisi  Suleiman Bishanga amesema hayo tarehe 19 Machi 2024; alipozungumza na Kipindi cha TANROADS Mkoa kwa Mkoa kuhusu mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita katika sekta ya ujenzi wa miundombinu ya barabara,  madaraja na viwanja vya ndege.

 

Mha. Bishanga amesema ujenzi wa barabara hiyo ya njia nne unajengwa .kwa utaratibu wa EPC + F na Mkandarasi M/s China Civil and Engineering Construction Coopration (CCECC) kutoka China, ambaye tayari ameshaanza maandalizi ya kuainisha maeneo ya kujenga kambi.

 

Amesema pia mradi huo utakuwa na barabara za mchepuo (Bypass), ili kuondoa msongamano wa magari hususan malori ya mizigo katikati ya mji.

 

Amesema miradi mingine ambayo ipo kwenye mipango ya serikali katika ujenzi ni pamoja na barabara ya Mlowo – Kamsamba na Spur ya Chitete Makao Makuu ya Wilaya ya Momba (Km 147), ambapo tayari ujenzi wa daraja la Momba linalounganisha Mkoa wa Songwe na Rukwa umekamilika

 

Mradi mwingine ni barabara ya Isongole II – Ngana/Mbeya – Kasumulu hadi Katumbosongwe (Km 124), sehemu ya Kwanza ya Isongole II – Ibungu – Isoko (Km 52.419) ujenzi unatarajia kuanza hivi karibuni kwa kiwango cha lami baada ya kukamilika kwa zabuni na mkandarasi kutangazwa na ulipaji wa fidia wa mali, nyumba na mazao umeshakamilika ambapo waathiriwa wa mradi wapatao 312 wamelipwa jumla ya kiasi cha Tshs.  Milioni 850.269.

 

Barabara nyingine ni ya Ruanda – Nyimbili – Izilya – Itumba (Km 79) na Mahenje – Haasamba – Vwawa Km 32. Sehemu ya kwanza km 1.2 Mkandarasi aitwae GNMS Contractors C. Ltd kutoka Iringa anaendelea na kazi; sehemu iliyobaki ya Ruanda – Idiwili km 20 imetengwa sehemu nne za km 5 kila moja kwa kiwango cha lami zitakazosimamiwa na Wakandarasi Wanawake.

 

Mha. Bishanga ametaja mradi mwingine ni barabara ya Mbalizi – Chang’ombe – Mkwajuni – Saza – Patamela hadi Makongorosi Km 110, Sehemu ya Chang’ombe – Mkwajuni – Saza – Patamela hadi Makongorosi Km 61, Barabara ya Ibungu – Kafwafwa na Itumba – Shigamba – Ibaba – Katengere pamoja na Ujenzi wa madaraja mawili ya Magamba na Namkukwe katika barabara ya Galula – Namkukwe (Km44.3).