News

Miradi mitatu ya barabara za lami yenye jumla ya Km.111.4 yakamilika mkoani Mara

Miradi mitatu ya barabara za lami yenye jumla ya Km.111.4 yakamilika mkoani Mara

Mara

13 Machi, 2024

Serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imekamilisha miradi mitatu ya ujenzi wa barabara zenye jumla ya  Kilomita 111.4  mkoani Mara.

Miradi hiyo ni ujenzi kwa kiwango cha lami katika barabara ya Nyamuswa - Bunda-Bulamba (Km 56.4), Makutano juu - Sanzante (Km 50)  na barabara ya Musoma – Busekela (Km 92), kipande cha kwanza cha kutoka Kusenyi - Suguti (Km 5).

Meneja wa TANROADS mkoa wa Mara, Mhandisi Vedastus Maribe amesema hayo tarehe 13 Machi 2024 alipozungumza na Waandishi wa Habari kuhusu mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita katika sekta ya ujenzi.

“Tunaishukuru serikali yetu chini ya Mama yetu, Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kutoa kiasi cha shilingi Bilioni 137.165 ili kutekeleza mradi wa barabara hizi tatu ambazo ujenzi wake umekwishakamilika” amesema Mha. Maribe

Amesema kufunguliwa kwa barabara hizo kumeongeza uchumi wa mkoa kwa kurahisisha usafiri kwa watalii wanaokuja nchini kuelekea katika mbuga ya Serengeti, pia zimechochea fursa kwa wafanyabishara wa madini kuweza kuuza madini yao katika soko la kimataifa pamoja na  kurahisha  huduma ya usafiri wa kutoka mkoa wa Mara kwenda mikoa jirani kwa uharaka zaidi tofauti na ulivyokuwa awali.

Ametaja miradi mingine inayoendelea kujengwa kwa kiwango cha lami ni barabara ya Sanzante- Nata (Km 40), Mogabiri-Nyamongo (Km 25), Tarime-Mugumu- (Km 87.14) sehemu ya Tarime-Mogabiri (Km 9.3), Nyamongo-Mugumu (Km 48.15), na barabara ya mzunguko ya Mugimu (Km 3.6), ukarabati na upanuzi wa Kiwanja cha ndege cha Musoma, pamoja na Ujenzi wa mizani ya kupima magari yakiwa kwenye mwendo.

Pia, ameishukuru serikali kwa kuwajali wakandarasi wazawa kwani miradi yote ya
matengenezo ya barabara imefanywa na wakandarasi hao ikiwa ni juhudi za serikali za  kuwajengea. uwezo.

Mha. Maribe amesema mradi mwingine ni usimikaji wa taa zaidi ya 608 za barabarani zikiwa zimefungwa katika maeneo ya Musoma mjini, Bweri, Nyabange, Butiama, Kiabakari, Sabasaba, Pida, Utegi, Mika, Mazami, Makutano (ziroziro) pamoja na Nyanchabakenye na mwaka huu zitasimikwa taa nyingine zaidi ya 336 kwenye maeneo ya Kusenyi, Musoma Manispaa, Nyamuswa, Komaswa, Bitaraguru, Nyamika na Olio.