News

Serikali ya Awamu ya Sita yaendelea kuufungua mkoa wa Ruvuma kwa barabara, madaraja na viwanja vya ndege

Serikali ya Awamu ya Sita yaendelea kuufungua mkoa wa Ruvuma kwa barabara, madaraja na viwanja vya ndege

Ruvuma,

14 Machi, 2024

Serikali ya awamu ya sita kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), inaendelea na jitihada za kuhakikisha kuwa miundombinu ya barabara na madaraja mkoani Ruvuma inaimarishwa, ili kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji wa watu na bidhaa mbalimbali kwa ajili ya kuinua Uchumi na kupunguza umaskini.

Katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Serikali imeendelea na utekelezaji wa miradi mikubwa ya ujenzi wa barabara, madaraja na viwanja vya ndege, ikiwa ni pamoja na barabara Mbinga – Mbambabay Km 66 ambayo imekamilika na ujenzi wa daraja la Ruhuhu lenye urefu wa mita 98.01 linalounganisha Wilaya za Nyasa mkoani Ruvuma na Wilaya ya Ludewa mkoani Njombe.

Akizungumza na Waandishi wa Habari tarehe 14 Machi 2024, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Salehe Juma Mkwama amesema serikali imefanya ukarabati na ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Songea na inaendelea na ujenzi wa barabara ya Kitai -Lituhi - Ndumbi Km 95. 3 inayokwenda Bandari ya Ndumbi, ambayo pia inatumika kusafirisha makaa ya mawe, ambapo inajengwa kwa kiwango cha lami.

Amesema kutokana na kutumika muda mrefu na hivyo kuchakaa serikali ipo mbioni kujenga upya barabara ya Songea – Makambako Km 295 na imekusudia kujenga daraja la Mitomoni, barabara ya Likuyufusi hadi Mkenda Km 124 ikijumuisha ujenzi wa daraja la Mkenda linalounganisha nchi ya Tanzania na Msumbiji katika mto Ruvuma na ujenzi wa barabara ya Lupiro – Malinyi – Kilosa kwa Mpepo – Londo – Kitanda – Lumecha Km 512 ambayo inaunganisha mikoa ya Ruvuma na Morogoro.

Mha. Salehe amesema pia serikali kupitia TANROADS imefanya usanifu katika barabara za Mbamba bay – Lituhi Km 112.4, barabara ya Mtwarapachani – Nalasi – Tunduru Km 300, barabara ya Unyoni – Maguu – Kipapa Km 25, barabara ya Nangombo – Chiwindi Km 40, na barabara ya Madaba – Mundindi (Liganga) – Mkiu Km 35.

Ameongeza kuwa TANROADS mkoa wa Ruvuma inasimamia mizani nne kwa ajili ya kudhibiti magari yasizidishe uzito na kuharibu barabara, ambazo zipo katika vijiji vya Lipokela kwenye barabara ya Songea – Mbinga, Luhimba kwenye barabara ya Songea – Lukumburu, Sisi kwa Sisi kwenye barabara ya Tunduru – Lumesule na Kijiji cha Buruma.