Ujuzi wa rasilimali watu kigezo cha uzalishaji wenye tija
*Yasisitizwa mkazo usiwekwe kwenye ufaulu wa taaluma pekee
Dar es Salaam
10 Machi, 2024
MTENDAJI Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Mohammed Besta, amesema rasilimali watu ni nyenzo muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi katika nchi yoyote, hivyo inahitaji kujengewa uwezo, hasa kwenye eneo la ujuzi na maarifa.
Mhandisi Besta anaunga mkono mikakati ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika kuinua wakandarasi wazawa nchini, kwa kuwajengea uwezo na uzoefu kwenye maeneo mbalimbali, ikiwemo ujuzi wa kitaalamu na maarifa.
Akizungumza Dar es Salaam hivi karibuni, Mhandisi Besta alisema kuna uhusiano mkubwa kati ya uwezo wa kiutendaji wa rasilimali watu iliyopo katika taifa, unaojumuisha ujuzi, maarifa; na uzalishaji wenye tija.
Alisema nchi au taifa lolote likitaka kufikia maendeleo ya kiuchumi, lazima lijali, litunze na kuiendeleza rasilimali watu iliyonayo hasa kwa kuwekeza katika eneo la ujenzi wa ujuzi na maarifa yake.
"Ujenzi wa uwezo katika ujuzi na maarifa ya rasilimali watu haupaswi kubagua taaluma, kwa sababu uchumi wa nchi unajengwa na watenda kazi kutoka katika fani (taaluma) nyingi tofauti, na wala haujengwi na fani moja.
Kwa mujibu wa Mhandisi Besta, utaratibu uliopo sasa wa kujali na kuthamini sana ufaulu katika taaluma unapaswa kuzungumzwa upya, ili kuchochea mabadiliko.
Aliweka wazi kuwa Tanzania, kama ilivyo mahali kwingine Afrika, imekwisha kumbwa na tatizo la baadhi ya watu wake kukosa ujuzi na maarifa katika mambo kadha wa kadha, hivyo kutofikia viwango vya uzalishaji wenye tija', vinavyotakiwa
Aidha, alisema taifa lolote likitaka kuyafikia maendeleo ya kiuchumi yaliyo kusudiwa, ni lazima lijitafakari kuona kama lina mikakati yoyote ya kukuza uwezo wa rasilimali yake katika eneo la ujuzi na maarifa.
"Ikiwa mikakati hiyo haipo ni vyema ikaandaliwa programu na miundo itakayosapoti kuendelezwa au kujengewa uwezo kwa rasilimali watu,"alisema.