Barabara ya Kimara - Bonyokwa - Kinyerezi kujengwa kwa kiwango cha lami ndani ya miezi 16
Dar es Salaam
09 Machi, 2024
Serikali kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imemkabidhi Mkandarasi kazi ya ujenzi wa Barabara ya Kimara – Bonyokwa – Kinyerezi kwa kiwango cha lami; Sehemu ya kwanza yenye urefu wa kilomita 6 pamoja na ujenzi wa daraja la Kinyerezi lenye urefu wa mita 25.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi Mhe. Innocent Bashungwa kwenye hafla iliyofanyika kwenye eneo la mradi tarehe 9 Machi 2024, Mkuu wa Mkoa wa Dar - es Salaam Mhe. Albert Chalamila amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kusikia kilio cha miaka mingi cha wakazi wa Jimbo la Ubungo na Segerea ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakilalamikia ubovu wa barabara hiyo ambayo wamesema ilikuwa kikwazo cha maendeleo katika eneo hilo.
RC Chalamila amemtaka Mkandarasi wa kampuni ya kizawa ya Nyanza Road Works iliyopewa kazi ya ujenzi wa barabara hiyo kufanya kazi usiku na mchana ili ikiwezekana hata kabla ya mienzi 16 ambayo iko kwenye mkataba iwe imekamilika na kuhakikisha anazingatia viwango na thamani ya fedha iliyoelekezwa na Serikali katika utekelelezaji wa mradi huo ( value for Money).
Akizungumza kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa TANROADS Mha. Mohamed Besta; Mkurugenzi wa Miradi TANROADS Mha. Japharson Nnko amesema mkataba wa ujenzi wa Barabara hiyo ulisainiwa tarehe 9 Februari mwaka huu 2024 na kilichofanyika ni kumkabidhi rasmi mkandarasi eneo la mradi ili aanze kazi baada ya kuwa amekamilisha taratibu zote zinazotakiwa.
Amemtaka Mkandarasi huyo kufanya kazi kwa ueledi mkubwa ili kazi hiyo ikamilike kwa viwango la gharama zilizokubaliwa ikiwa ni pamoja na kuzingatia muda wa miezi 16 ya utekelezaji wa mradi kwani kwa mujibu wa Mkataba anatakiwa amalize kazi hiyo ifikapo tarehe 8 Julai 2025
Aidha ujenzi wa barabara hiyo ya kiwango cha lami inayojengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 24 ikihusisha pia mifumo ya maji, daraja, makaravati na kuwekwa taa za barabarani kwenye eneo lote la Barabara unaoanza rasmi leo tarehe 10 Machi 2024, ukikamilika utawezesha wakazi wa eneo hilo kufanya Shughuli za kiuchumi masaa 24