News

Barabara za mkoa wa Tanga kuunganisha nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki

Barabara za mkoa wa Tanga kuunganisha nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki

 

Tanga

Machi 4, 2024

Serikali ya awamu ya Sita kupitia (TANROADS) inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati ya ujenzi wa barabara Mkoani Tanga ambayo ikikamilika itaunganisha Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuchochea ukuaji wa uchumi ikiwa ni pamoja na kupunguza gharama na muda wa safari na kurahisisha ufanyaji biashara.

Pia itawezesha wananchi kuchangamana kwa urahisi, kuwezesha kufikika kwa urahisi kwenye vivutio vya utalii, kuwa kiungo kizuri kati ya bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mombasa na hivyo kuchochea uchumi wa Buluu.

Akuzungumza na Waandishi wa Habari tarehe 4 Machi 2024; Meneja wa TANROADS Mkoa wa Tanga Mha. Dastan Singano amesema miradi hiyo ni pamoja na ule wa ujenzi wa kiwango cha lami Barabara ya Bagamoyo (Makurunge) – Mkange – Pangani – Tanga yenye jumla ya urefu wa kilomita 256 ambayo ni sehemu ya Barabara ya Jumuiya ya Afrika Mashariki inayounganisha nchi mbili za Kenya na Tanzania kwa ukanda wa Pwani.

Mwingine ni Ujenzi wa barabara ya Handeni – Kiberashi – Kijungu – Chemba – Kwamtoro – Singida (km 434.33) kwa kiwango cha lami, ambao unatekelezwa na Serikali ya awamu ya Sita Chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa awamu; awamu ya kwanza ni ya ujenzi wa Sehemu ya Handeni – Mafuleta km 20; awamu ya pili, ujenzi wa Sehemu ya Mafuleta – Kileguru km 30 na awamu ya tatu ni kutoka Kileguru – Kiberashi – Kijungu – Chemba – Kwamtoro – hadi Singida km 384.33 ambayo itajengwa kwa mfumo wa EPC+F.

Akizungumzia mradi wa Bagamoyo (Makurunge) – Mkange – Pangani – Tanga Mha. Singano amesema unatekelezwa katika sehemu nne, Sehemu ya Kwanza Tanga – Pangani (Km 50), Sehemu ya Pili, Daraja la Mto Pangani lenye urefu wa mita 525 na  barabara unganishi za maingilio ya daraja zenye jumla ya urefu wa km 14.3, barabara ya Ushongo km 5.9 na Barabara za Pangani mjini zenye urefu wa km 5.4, na Sehemu ya tatu ni Mkange – Mkwaja – Tungamaa km 95.2, ikijumuisha barabara unganishi ya Kipumbwi yenye urefu wa km 3.7 ( Sehemu ya nne bado haijaanza).

Ameeleza "Kwa upande wa barabara ya Tanga – Pangani ujenzi ulikuwa unasuasua lakini baada ya Mhe. Rais Samia kutoa fedha mwezi Januari 2024 zimemfanya Mkandarasi kupata nguvu ya kutekelezaji mradi ule kwa kasi’’.

Amesema pia Serikali ya awamu ya sita  ina mpango wa kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya Mkata – Kwa Msisi km 36, barabara ya kutoka Old Korogwe kwenda Bombomtoni mpaka Mabokweni km 127, barabara ya Soni - Bumbuli – Dindira – Korogwe km 30 na barabara ya Handeni kwenda Mziha ambayo tayari Serikali imeshatoa kibali  cha kuanza ujenzi wa km 20.

“Kwa kweli hizi ni juhudi za pekee anazozifanya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha mtandao wetu wa barabara Tanga unakuwa vizuri, tunamshukuru sana, kwa sababu yeye kwa kuleta fedha za utekelezaji wa miradi hii imeleta fursa, kuna ajira ambazo zimezalishwa ambazo wamezipata Watanzania" amesisitiza.