News

Rais Dkt. Samia adhamiria kuufungua kiuchumi mkoa wa Manyara kwa ujenzi wa barabara za lami

Rais Dkt. Samia adhamiria kuufungua kiuchumi mkoa wa Manyara kwa ujenzi wa barabara za lami

 

Manyara

Machi 3, 2024

Serikali ya Awamu ya sita chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuinua Uchumi wa Wananchi na pato la Taifa kwa kuufungua Mkoa wa Manyara kwa ujenzi wa barabara za lami ambazo zitaunganisha Uchumi wa Kanda ya ziwa na Nchi Jirani za Burundi, Uganda na Rwanda kwa kutumia Bandari ya Tanga.

 

Miradi mitatu kati ya saba mikubwa ya Kitaifa ya ujenzi wa barabara ambayo tayari Serikali kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) ilishasaini mikataba kwa ajili ya ujenzi itapita katika Mkoa wa Manyara.

 

Meneja wa TANROADS Mkoa wa Manyara Mhandisi Dutu J. Masele amebainisha hayo alipohojiwa na Waandishi wa Habari kuhusu mafanikio ya miaka mitatu ya Serikali ya awamu ya sita katika sekta ya ujenzi wa Miundombinu.

 

Amesema miradi hiyo inayotekelezwa kwa kushirikiana na wabia kwa mfumo wa EPC + F inaanzia Handeni Mkoani Tanga – Kiteto Manyara – Chemba Dodoma hadi Singida, katika mradi huo Mkoa wa Manyara una jumla ya Kilomita 120, mradi mwingine ni ule unaounganisha Mkoa wa Dodoma – Manyara na Arusha (Arusha – Kibaya – Kongwa) Mkoa wa Manyara una jumla ya Kilomita 333.

 

Mradi wa tatu ni Karatu, Mbulu, Haydom, Sibiti, Lalago – Maswa kilomita 389, kilomita 50 zilizopo katika Mkoa wa Manyara tayari zipo kwenye utaratibu wa ujenzi na zinajengwa kwa fedha za ndani kwa maelekezo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

 

Ameongeza kuwa “Tumpongeza Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia kuona namna ambavyo anaenda sasa kuufungua Mkoa wa Manyara kwa maana katika miradi yote saba yenye jumla ya Kilomita 2035 itakayotekelezwa Nchi nzima kwa utaratibu wa EPC + F; Kilomita 515 ipo katika Mkoa wa Manyara’’.