News

TANROADS kujenga madaraja makubwa ya Chakwale na Nyuyami katika barabara ya Kilosa

 

TANROADS kujenga madaraja makubwa ya Chakwale na Nyuyami katika barabara ya Kilosa

 

Morogoro

22 Februari,2024

Serikali kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imekusudia kujenga madaraja mawili makubwa ya Chakwale na Nyuyami ambayo yamekuwa changamoto kipindi cha mvua kubwa katika barabara ya kimkakati ya Gairo – Nongwe Mkoani Morogoro.

Waziri wa Ujenzi Mhe. Innocent Bashungwa amesema hayo tarehe 22 Februari 2024; katika ziara yake ya kikazi Mkoani Morogoro ambapo alikagua madaraja hayo mawili kisha kuzungumza na Wananchi wa maeneo hayo na kuwaeleza utekelezaji wa miradi hiyo ni sehemu ya dhamira ya dhati ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuendelea kujenga na kuboresha miundombinu ya barabara na madaraja kote Nchini.

Amesema tayari Serikali imeshatoa fedha ambazo zimeiwezesha TANROADS kufanya usanifu wa kina hivyo baada ya usanifu Mhe Rais Dkt. Samia anakwenda kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa madaraja makubwa ya kisasa ya Chakwale na Nguyami,  ambayo yataenda sambamba na mahitaji ya barabara hiyo ambayo inaunganisha Mkoa wa Morogoro na Tanga.

“Madaraja tunayoenda kujenga hapa yatakuwa ni ya viwango ili lami itakapokuja madaraja hayo hayo yatumike, kwa usanifu ambao umefanyika na ukubwa wa madaraja haya ndugu zangu wakati wa Sendoff na harusi mtakuwa mnakuja kupiga picha hapa mnapendeza kabisa, Serikali ya Dkt Samia ni Serikali ya vitendo tumekuja hapa baada ya kujua hapa tunahitaji gharama kiasi gani na madaraja ya urefu kiasi gani, nimekuja hapa ili mjue kile ambacho mlikuwa mnakililia na Seikali ya awamu ya sita na Chama cha Mapinduzi tumewasikia’’ ameeleza.

Kwa upande wake Meneja wa TANROADS wa Mkoa wa Morogoro Mhandisi Alinanuswe L. Kyamba amesema ujenzi wa daraja la Chakwale utakuwa na urefu wa mita 80 na daraja la Nyuyami litakuwa na urefu wa mita 100 na kukamilika kwa miradi hiyo kutasaidia kuchochea ukuaji wa uchumi wa Wananchi wa Wilaya ya Gairo, Mkoa Morogoro na maeneo ya Jirani.

Naye Mbunge wa Gairo Mbunge wa Jimbo la Gairo Mhe. Ahmed Shabiby amesema barabara hiyo ina madaraja sumbufu matatu ikiwemo hayo mawili na moja la Matale ambao linahitaji Makalvati …  "sio kubwa kama hayo mawili, tunashukuru TANROADS kwa kuwa wameyajenga mengi kwa kiwango kizuri kabisa kwamba yawe madaraja ya kudumu”