News

BARABARA YA TANGA - KILOSA - MIKUMI - LUPEMBE KUPANDISHWA HADHI KUWA BARABARA KUU “TRUNK ROAD”

BARABARA YA TANGA - KILOSA - MIKUMI - LUPEMBE KUPANDISHWA HADHI KUWA BARABARA KUU “TRUNK ROAD”

Tanga

24 Februari, 2024
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amemuelekeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi kuipandisha hadhi barabara ya Tanga - Kilosa - Mikumi - Lupembe kuwa barabara kuu 'Trunk Road' ili kuinua uchumi wa mikoa ya Tanga, Morogoro na Njombe.


Bashungwa, ameyasema hayo mkoani Morogoro wakati akikagua ujenzi wa barabara ya Dumila-Kilosa-Ulaya-Mikumi (km 142) kwa kiwango cha lami sehemu ya pili, Rudewa-Kilosa (km 24), ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 98.


“Barabara inayoanzia Tanga bandarini kupitia Handeni - Mziha - Dumila - Kilosa - Mikumi - Ifakara mpaka Lupembe mkoani Njombe lazima tuitangaze iwe ni mojawapo ya barabara kuu ‘Trunk road’ ili iweze kuipatiwa bajeti ya kutosha na kuweza kuihudumia wakati wote”, amesema Bashungwa.

Aidha, Bashungwa amemtaka Mkandarasi M/s Umoja - Kilosa Jv anayetekeleza mradi huo kufanya kazi usiku na mchana na kuhakikisha barabara na madaraja yanakamilika kwa wakati kama ilivyopangwa kwenye mkataba kwani fedha zote zimeshalipwa na ifakapo mwezi wa nne mwishoni waikabidhi barabara hiyo.


Bashungwa akijibu ombi la Mbunge wa Kilosa, Prof. Palamagamba Kabudi la uwekaji wa taa, amesema Wizara itatenga bajeti ya ufungaji wa taa 120 katika kipande cha kilometa tatu katika barabara ya Rudewa - Kilosa.


Aidha, Waziri Bashungwa amemuelekeza Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania  (TANROADS) Mkoa wa Morogoro kuhakikisha wanatenga bajeti za matengenezo ya upanuzi wa njia ya maji katika mito yote ili mvua zitakaponyesha zisilete athari kwenye miundombinu ya barabara.


Akitoa taarifa ya mradi kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Kaimu Mkurugenzi wa Usimamizi wa Miradi, Mhandisi Malima Kusesa, amesema mradi wa ujenzi wa barabara hiyo ni kwa kiwango cha lami sehemu ya pili, Rudewa-Kilosa (Km 24) umefikia asilimia 98.3 na sehemu iliyobaki ni ujenzi wa madaraja matatu ambayo yanaunganisha barabara hiyo.Vilevile ameongeza kwa kusema kuwa mradi huo unafadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa asilimia 100.


Kwa upande wake Mbunge wa Kilosa, Profesa Kabudi, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutekeleza ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami kwani muhimu katika uchumi wa wana Kilosa na Tanzania kwa ujumla.


Utekelezaji wa mradi huo ni moja ya mkakati wa Serikali katika kukuza uchumi  na kuunganisha mikoa ya Kaskazini (Tanga, Kilimanjaro na Arusha) na Mikoa ya Kusini (Iringa, Mbeya na Ruvuma) kupitia Turiani na Mziha.