News

Tanzania na Misri wapanga mikakati ya ushirikiano

Tanzania na Misri wapanga mikakati ya ushirikiano

 

Na Mwandishi Wetu

SERIKALI za Tanzania na Misri zimepanga mikakati mikubwa ya ushirikiano katika Sekta ya Ujenzi wa miundombinu ya barabara, madaraja, nyumba, ufundi na umeme.

 

Akizungumza mara baada ya kikao cha pamoja kilichofanyika leo tarehe 20 Februari, 2024 jijini Dar es Salaam, Waziri wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa na Waziri wa Uchukuzi wa Misri, Luteni Jenerali Kamel Alwazeer, pamoja na ujumbe wake uliofanyika Jijini Dar es Salaam, amesema wameweka vipaumbele kadhaa vya ushirikiano utakaoleta tija kwa nchi zote mbili.

 

Mhe. Bashungwa amesema wamezungumzia ukarabati wa kiwango bora cha barabara ya kutoka Misri hadi kwenye mji wa Capetown, Afrika ya Kusini, ambapo kipande cha barabara hiyo chenye urefu wa kilometa 1600 kitapita Tanzania.

 

“Ninamshukuru sana Rais wetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kufungua nchi yetu na kuimarisha mahusiano kati ya nchi yetu na nchi mbalimbali, kama hapa tumepata ugeni kutoka kwa wenzetu wa nchi ya Misri wakiongozwa na Waziri wa Uchukuzi ili kujadiliana namna ya kusaidiana kimkakati katika masuala ya ujenzi wa miundombinu, ikiwemo ya ukarabati wa barabara inayotoka nchi ya Misri hadi mji wa Capetown nchini Afrika Kusini na itapita kwa asilimia kubwa ndani ya nchi yetu,” amesema Mhe. Bashungwa.

 

Mhe. Bashungwa amesema barabara hiyo itakayounganisha Afrika kwa kupita katika nchi tisa ikitoka Misri kwa hapa Tanzania itapita kwenye mikoa ya Songwe, Mbeya, Iringa, Dodoma, Manyara, Arusha hadi mji wa Namanga; wakati kwa nchi za Afrika itapita ni pamoja na Burundi, Rwanda, Uganda, Kenya, Malawi, Msumbiji, Kongo, Afrika ya Kusini  na Zambia.

 

Amesema wamekubaliana na Wizara hii kukutana na kukaa pamoja ili kuona namna bora ya kufanya ukarabati wa hali ya juu kwa kipande cha barabara hiyo kinachopita Tanzania utakavyokuwa, ambapo wameweka mkakati wa kufanikisha mazungumzo hayo kwa haraka, huku akiwataka Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), kukaa na wataalamu ili wajadili muundo bora wa ujenzi wa barabara hiyo, na namna ya upatikanaji wa fedha za ujenzi..

 

Hatahivyo, amesema kukamilika kwa barabara hii kutaonesha jitihada za dhati zinazofanywa na Mhe. Rais Samia za kutekeleza Ilani ya Chama tawala na kufanya uchumi wa nchi ukue kutokana na kuwa na miundombinu bora.

 

Pia amesema wamekubaliana mashirikiano kwa upande wa wahandisi wanaomaliza masomo yao ya vyuo vikuu, ili waweze kupata ujuzi na uzoefu zaidi kwa kwenda kufanya kazi kwenye miradi ya ujenzi itakayokuwa hapa nchini, ambapo tayari amewaagiza TANROADS, kuhakikisha wanaongeza kipengele cha kuwataka Wakandarasi wanaopata kandarasi za kufanya kazi hapa nchini, mbali na kutumia wahandasi waliokuja nao, lazima pia wawajumuishe wahandisi wahitimu kutoka vyuo mbalimbali nchini.

 

Naye Waziri wa Uchukuzi wa Misri, Luteni Jenerali Kamel Alwazeer amesema anamshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia kwa kuwapa mwaliko wa kutembelea Tanzania, na kuangalia fursa za uwekezaji, ambapo pia amewakaribisha Wizara ya Ujenzi kutembelea nchini Misri ili kujionea ujenzi wa barabara na madaraja ya kisasa.

 

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta amesema kwa kuwa wakala hiyo inajukumu kubwa la ujenzi wa barabara, hivyo wapo tayari kwa utekelezaji mara ujenzi wa barabara hiyo utakapoidhinishwa na serikali kama ilivyokuwa awali kwa nyingine.

 

Mkutano huo pia umeudhuriwa na wataalam na Wakurugenzi kutoka Wizara ya Ujenzi, TANROADS, Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) na Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA)

MWISHO.