News

TANROADS MKOA WA TABORA IMEWATAKA WANANCHI KUACHA KUVAMIA MAENEO YA HIFADHI YA BARABARA

 
 
TANROADS MKOA WA TABORA IMEWATAKA WANANCHI KUACHA KUVAMIA MAENEO YA HIFADHI YA BARABARA
 
TABORA
19 Februari, 2024
Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Tabora imetoa wito kwa Wananchi kuacha tabia ya kuvamia na kufanya shughuli za kibinadamu ikiwemo kilimo na kujenga vibanda vya biashara kwenye maeneo ya hifadhi ya barabara kwani kufanya hivyo ni kinyume cha sheria na kunasababisha uharibu mkubwa katika miundombinu ya barabara ambayo inajengwa na Serikali kwa gharama kubwa.
 
Akizungumza na kipindi cha TANROADS Mkoa kwa Mkoa leo tarehe 18 Februari 2024; Meneja wa TANROADS Mkoa wa Tabora Mhandisi Raphael S. Mlimaji ametaja athari za kufanya shughuli za kibinadamu hasa kilimo kwenye hifadhi ya barabara ni pamoja na kusababisha mmomonyoko wa udongo ambao unaweza kubababisha  barabara kukatika muda wowote na kuisabibishia Serikali hasara ya kufanya tena matengenezo ya kufukia mashimo na kujenga miundombinu ambayo imeharibiwa.
 
Amesema hifadhi za barabara zinazosimamiwa na TANROADS kwa ujumla wake katika Mkoa wa Tabora ni kilomita za mraba 131.29 maeneo ya barabara yaliyoathiriwa kilomita za mraba 105. 98 na eneo ambalo halijaathiriwa ni kilomita za mraba 25.5 na eneo ambalo halijaathiriwa ni yale mapori tengefu ambayo Wananchi wamekuwa wakiyaogopa sana kuliko maeneo mengine.
 
 "Tulichofanikiwa Mkoa wa Tabora ni kuondoa vibanda vilivyokuwa kwenye hifadhi ya barabara, sasa imebidi tuchukue tahadhari mapema, kwamba watu waepuke kuvamia hifadhi ya barabara kwa namna yoyote ile; kwani unaporuhusu watu kujenga kwenye hayo maeneo kunaweza kuiingiza Serikali kwenye hasara kwa sababu barabara husika itakapohitaji upanuzi unaweza kujikuta unalipa fidia watu ambao hawastahili''. ameeleza.
 
Mha. Raphael Mlimaji ameongeza kuwa  Sheria namba 13 kifungu cha 29 ibara ndogo ya 1 mpaka 4, A na B inaelekeza matumizi sahihi ya barabara, kifungu cha 48 cha sheria hiyo kinaeleza hatua anazoweza kuchukuliwa mtu anayefanya shughuli za kibidamu kwenye hifadhi ya barabara ikiwemo kukamatwa na kufikishwa mahakamani ambapo anaweza kulipishwa faini, kufungwa jela mpaka miaka mitatu ama vyote kwa pamoja.