News

BASHUNGWA ATAKA MUAROBAINI WA BARABARA KUHARIBIKA KABLA YA MUDA

BASHUNGWA ATAKA MUAROBAINI WA BARABARA KUHARIBIKA KABLA YA MUDA

 

DODOMA

15 Februari, 2024

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amewaagiza Wakala ya Barabara Tanzania  (TANROADS), kutafuta ufumbuzi kuhusu suala la  kuharibika kwa barabara kabla ya muda uliopangwa ili kuokoa fedha za Serikali zitakazotumika kurekebisha miundombinu hiyo.

 

Agizo hilo amelitoa jijini Dodoma Februari 14, 2024 katika kikao cha 19 cha Baraza la  Wafanyakazi wa  TANROADS na kuwasisitiza kusimamia miradi kwa weledi na  uzalendo ili kusaidia miradi kukamilika kwa viwango na kwa wakati.

 

“Suala  la  kuharibika kwa barabara kabla ya wakati ‘pre-mature failure’ ni tatizo,  hakikisheni mnapambana  nalo,  chukueni hatua za kisheria kwa Mkandarasi atakayetekeleza mradi chini ya kiwango”,  amesema Bashungwa.

 

Aidha,  Bashungwa ameagiza  TANROADS  kutumia kikamilifu mtambo wa Ukaguzi wa Barabara  (Road  Scanner)  wakati wakufanya ukaguzi wa miradi ya barabara na madaraja na hata kutumia vifaa vingine vitakavyoweza kuwasaidia kubaini ubora wa mradi mapema kabla ya kukabidhiwa.

 

Ameielekeza TANROADS kuimarisha na kukijengea uwezo Kitengo chake cha Usimamizi wa miradi (TECU), ili kusimamia miradi kwa weledi na ufanisi.

 

Kadhalika, Bashungwa ameitaka TANROADS kusimamia sheria ya uzito wa magari barabarani na kutoa faini au adhabu nyingine kwa yeyote atakayekiuka sheria hiyo kwa mujibu wa sheria pamoja na kuwaelekeza Maafisa wanaofanyakazi kwenye mizani kutii na kufuata sheria kama inavyoelekeza ili kuzilinda barabara nchini.

 

“Hakuna kiongozi wala mtumishi ambaye yupo juu ya sheria,  hata mimi siwezi kumsaidia yeyote anayekiuka sheria hii,  atakayekiuka achukuliwe hatua na sio kunipigia simu”,  amesema Bashungwa.

 

Bashungwa amesisitiza umuhimu wa Wakala huo kuwajengea uwezo Wataalam wake  ikiwemo katika eneo la usimamizi wa miradi na mikataba ili kuleta tija kwa TANROADS na Taifa kwa ujumla.

 

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta,  amemhakikishia  Waziri  Bashungwa kutekeleza maagizo aliyowapa na kuendelea kufanyakazi kwa ari na bidii katika utendaji wao wa kila siku ili kuleta tija kwa Wakala huo.

 

Naye, Mweyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Migodi, Nishati, Ujenzi na kazi nyingine (TAMICO), Mhandisi  Nchama Wambura,  amesema wataendelea kushrikiana na kufanyakazi kwa bidii ili kuleta mabadiliko chanya na maendeleo kwa utekelezaji sahihi na ubora kwa miradi wanayoendelea kutekeleza nchini.

 

Mkutano wa 19 wa Baraza la wafanyakazi la TANROADS, umefanyika Dodoma kwa Siku 2 na kushirikisha zaidi ya wajumbe 100 kutoka Mikoa yote nchini.