TANROADS yaja na mbinu mpya ya kujenga pango la kupita tembo kwenda kwenye hifadhi badala ya kukatiza juu ya barabara
MOROGORO
14/02/2024
Katika kuhakikisha miundombinu ya Barabara ya Kidatu – Ifakara yenye urefu wa kilometa 66.7 inakuwa imara na salama kwa watumiaji. Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imekuja na mbinu mpya ya kujenga pango lenye upana wa mita tano na kina cha mita 4.5 katika Kijiji cha Sonje ili kuwaepusha na ajali za magari Tembo wa Mbuga ya Wanyama ya Mwalimu Nyerere ambao kila mwaka hupita kwenye eneo hilo kuelekea Hifadhi ya Udzungwa.
Akizungumza hivi karibuni na Kipindi cha TANROADS Mkoa kwa Mkoa, Kaimu Mhandisi Mkazi wa Mradi wa barabara ya Kidatu – Ifakara kutoka TANROADS, Kitengo cha Wahandisi Washauri (TECU), Mhandisi Marcel Kiimu amesema kitu cha kutofautisha barabara hiyo na ujenzi wa miradi mingine ni uwepo wa pango hilo kwa Tanzania nzima halipo sehemu nyingine yeyote.
Amesema TANROADS kwa kushirikiana na Mkandarasi M/s Reynolds Construction Company kutoka Nigeria wamebuni njia hiyo baada ya kuona makundi ya Tembo yakitoka katika Mbuga ya Mwalimu Nyerere na kwenda Hifadhi ya Udzungwa kila mwezi Desemba hadi Februari kila mwaka, na baadaye kurudi katika mbuga hiyo waliyotoka awali.
Amesema katika eneo wanalopita tembo kumejengwa uzio na kuwekewa umeme wa kuwashtua ili wasiweze kusambaa kwenye mashamba na makazi ya wananchi na kuharibu mazao au kuleta maafa kwa wakazi hao, ambao wapo jirani na pango hilo.
Mha. Kiimu ameeleza kuwa pango hilo linauwezo wa kupitisha tembo wanne kwa wakati mmoja ambao watatokea upande wa pili, ambao pia wametengenezewa njia kuzunguka mlima wa kuelekea Udzungwa.
Kabla ya ujenzi wa pango hilo wanyama hao walikuwa wakipita katikati ya barabara na kusababisha adha kwa watumiaji wa barabara hiyo, pia kwa wakazi wa eneo hilo kujifungia ndani na kushindwa kuendelea na majukumu yao ya kila siku ikiwemo biashara na kilimo kwa kuhofia kupata madhara au kuuwawa na tembo hao.