News

DARAJA LA RUAHA MKUU KIDATU-IFAKARA KUUNGANISHA MIKOA MITANO NCHINI NA NCHI JIRANI

DARAJA LA RUAHA MKUU KIDATU-IFAKARA KUUNGANISHA MIKOA MITANO NCHINI NA NCHI JIRANI

 

Morogoro

13/02/2024

Imeelezwa kuwa Mradi wa Ujenzi wa Daraja la mto Ruaha Mkuu lililopo kwenye barabara ya Kidatu – Ifakara lenye urefu wa mita 133 mkoani Morogoro, utakapokamilika utakuwa na manufaa makubwa ikiwemo kuchagiza maendeleo, kukuza uchumi pamoja na kuunganisha mkoa huo na Mikoa mingine ya Iringa, Njombe, Ruvuma, Lindi na Mtwara na nchi jirani.

 

Akizungumza hivi karibuni Kaimu Mhandisi Mkazi wa Mradi huo unaokwenda sambamba na ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 66.9 kiwango cha lami, Mhandisi Marcel Kiimu amesema katika daraja hilo magari yatapita mawili ikiwa ni moja kila upande, tofauti na awali yalipita moja kwani ni jembamba hivyo limesababisha msongamano wa magari.

 

Amesema pia kwenye barabara hiyo kumejengwa kumejengwa madaraja mengine ya kawaida manne ambayo ni Ikela, Msolwa, Sumbugulu na Kisawasawa, makalavati makubwa 45 yenye urefu wa mita 584 kwa kila moja na makalvati ya kawaida 249, ambayo yote yatasaidia kupitisha maji kwa haraka.

 

Mradi huo wa kimkakati ni sehemu ya mkakati wa Taifa wa kuwasaidia wakulima wadogo wanaolima mazao ya chakula na biashara kupitia Programu ya uendelezaji Kilimo katika Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (SAGCOT), waliopo katika Bonde la Mto Kilombero, Ulanga, Mlimba na Malinyi.

 

Amesema barabara hiyo itakuwa na upana wa mita 9.5 ikiwa ni njia ya magari yenye upana wa mita 6.5 yenye lami nzito (asphalt concrete) na mabega ya barabara yenye upana wa mita 1.5 kwa kila upande wa maeneo yasiyokuwa na miji na upana wa mita 2.0 kila upande wenye miji, mitaro ya kupitisha maji na vivuko vya watembea kwa miguu.

 

Mha. Kiimu ameongeza kuwa mradi huo ujenzi wa barabara  ya Kidatu- Ifakara unaotarajiwa kukamilika Machi 2024 unasimamiwa na Kitengo cha TECU cha Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), ambapo utatumia gharama ya zaidi ya Shilingi Bil. 128.15, unawafanyakazi 792 kati yao wazawa ni 779 na 13 ni wageni, miongoni mwao wanaume ni 703 na wanawake ni 89. Pia kuna wahandisi wahitimu wa vyuo vikuu watano na wanafunzi toka vyuo vikuu saba