News

Watumishi wa TANROADS wapata mafunzo ya usalama katika matumizi ya TEHAMA

Watumishi wa TANROADS wapata mafunzo ya usalama katika matumizi ya TEHAMA

 

Dar es Salaam,

25 Januari, 2024

Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imewaweka tayari watumishi wake kwa kuwapa mafunzo ya usalama katika matumizi ya TEHAMA, ili waweze kukabiliana na uhalifu mtandaoni, mara watakapokutana nao.

 

Akifungua mafunzo ya siku tatu ya usalama katika kutumia TEHAMA mahala pa kazi na majumbani, yaliyoanza leo tarehe 25 Januari, 2024 yaliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa taasisi hiyo, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta amesema mafunzo haya ni takwa la sheria na sera ya Taifa ya masuala ya mpango mkakati wa mawasiliano (National Cybersecurity Communication Strategy, e-Transaction Act) ya mwaka 2015, na Sheria ya Usalama wa Taarifa Binafsi (Personal Data Protection) ya mwaka 2022 na kanuni mbalimbali.

 

Hatahivyo, amesema TANROADS ikiwa ni moja ya taasisi inamajukumu ya kutekeleza miongozo mbalimbali inayosimamia matumizi ya TEHAMA katika kufikisha huduma kwa jamii, pamoja nayo inakabiliwa na changamoto za uhalifu wa kimtandao, jambo ambalo linatishia usalama wa mifumo ya TEHAMA iliyopo.

 

Mha. Besta amesema  tayari taasisi hiyo imefunga mifumo wenzeshi ya TEHAMA ili kufanikisha utoaji huduma bora kwa wadau wake, ingawa sasa wanakabiliwa na changamoto hatarishi katika utoaji huduma kwa njia ya mtandao, kutokana na kukua kwa teknolojia na sasa kuna akili bandia, ambazo zinafanya kazi mbalimbali ikiwemo ya kuhatarisha taarifa, na mifumo ya taasisi, watu binafsi na wadau kwa ujumla.

 

Halikadhalika, amesema TANROADS imeanza kuchukua tahadhari kuhusiana na vihatarishi hivyo kwa kuanza kuwapa mafunzo ya ndani kwa watumishi wake, yatakayowajengea uwezo wa kukabiliana na changamoto hizo.

 

Kwa upande wake Meneja wa TEHAMA na Takwimu wa TANROADS, Bw. Majaliwa Mkinga amesema kwa wakala hii imesanifu mifumo wezeshi ya TEHAMA inayotumika kufanyakazi za kila siku, hivyo inapaswa kulindwa ili isipate madhara ya wahalifu wa mtandaoni.Bw. Majaliwa amesema kwa sasa dunia ipo katika mashambulizi mengi ya mfumo wa kimtandao, ambapo sasa mafunzo haya yatakayokuwa yakitolewa mara kwa mara yameanza na watumishi wa kitengo cha TEHAMA, na baadaye watafuata Menejimenti na watumishi wote ili kila mmoja aweze kupata mbinu za kukabiliana na changamoto hizo.