BILIONI 96 KUJENGA BARABARA YA LITUHI - BANDARI YA NDUMBI: WAZIRI BASHUNGWA
Serikali imetenga kiasi cha shilingi Bilioni 96 kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Lituhi kuelekea Bandari ya Ndumbi yenye urefu wa kilometa 50 kwa kiwango cha lami.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa leo tarehe 25 Januari 2025 wakati akizingumza na wananchi wa Lituhi mara baada ya kukagua barabara hiyo ambayo ipo katika hatua za kusainiwa mkataba.
Bashungwa amesema ujenzi wa barabara hiyo utawezesha meli za mizigo hasa makaa ya mawe ziweze kupakia kupitia Bandari ya Ndumbi kwenda sehemu mbalimbali za nchi yetu na nchi jirani za Malawi na Msumbiji.
Ameongeza kuwa barabara hiyo inaunganisha Mkoa wa Ruvuma na Njombe kupitia Daraja la Ruhuhu ambayo itafungua fursa za maendeleo na biashara.
Bashungwa ameagiza Wakala wa Barabara (TANROADS), kumsimamia Mkandarasi atakayepatikana kwa karibu ili mradi huo ukamilike kwa viwango.
Kwa upande wake, Mbunge wa Nyasa, Mhe. Eng. Stella Manyanya, amemuomba Waziri huyo kuwajengea angalau madaraja maeneo korofi hasa katika vipindi vya mvua kwani imekuwa Kero kwa wananchi wake.
Eng. Manyanya ameomba kipande cha barabara kutoka Mbambabay hadi Chiwimbi (km 45) ipewe kipaumbele kwa kuwa ni barabara muhimu na ya Ulinzi ambayo inaunganisha nchi ya Tanzania na Msumbiji, hivyo anaomba ipewe kipaumbele.
“Barabara ya kutoka Nyoni- Matomoni haimo kwenye ilani ila tulikuwa tunaomba ifanyiwe upembuzi yakinifu kwa sababu ni barabara ya uchumi, Kahama yote inatoka huko” ameongeza Eng. Manyanya.