Wananchi wapongeza jitihada za TANROADS kurejesha za mawasiliano Kunduchi- Mtongani
Dar es Salaam,
Januari 21, 2024
WANANCHI na Wakazi wa maeneo ya Kunduchi Mtongani, Bahari Beach, Ununio, Mbweni na Tegeta wamepongeza jitihada zilizofanywa na serikali kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) za kurejesha haraka mawasiliano ya barabara iliyokatika jana tarehe 20 Januari, 2024 baada ya kukatika kwa daraja la Mtongaji, kutokana na mvua kubwa za El-nino zinazoendelea nchini.
Wakazi hao wameyasema hayo leo tarehe 21 Januari, 2024 katika eneo la daraja la Mtongani wakishughudia wakandarasi wakiendelea na matengenezo ya haraka ili barabara hiyo iweze kutumika kama ilivyokuwa awali.
Bw. Fuya Godwin, mkazi wa Ununio amesema barabara hii ni kiunganishi kikubwa kati ya barabara mpya na ya zamani ya Bagamoyo (New na Old Bagamoyo road), ambapo imekuwa kimbilio kwa wakazi kwa kuwa haina foleni.
Amesema anaipongeza serikali ya awamu ya Sita ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, chini ya uongozi wake kwani watendaji wamekuwa makini na kufanya kazi kwa bidii na kutatua kwa haraka kero zinazowakabili katika jamii.
“Tunaishukuru sana serikali na Uongozi wa TANROADS kwa ujumla wake kwa hatua za haraka sana walizochukua, tunaridhika na kazi inayoendelea ilianza jana baada ya athari ya kukatika pamoja na mvua zinazoendelea lakini wanaendelea na kazi na tunaimani mawasiliano yatarejea kama zamani kwa haraka,” Amesema Bw. Godwin.
Naye Dkt. Donald Mmari mkazi wa Tegeta ameipongeza serikali kwa kujali wananchi na kujiweka tayari kwa dharura, ikiwemo ya kufanya matengenezo ya haraka ya barabara ya Bahari Beach ambayo ni muhimu na kiungo katika shughuli za uchumi na maendeleo.
Kwa upande wake Bi. Sakina Mkande, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Kanda ya Bahari Beach Kondo amesema kazi ya kurejesha mawasiliano ni kazi nzuri na yenye kuwapa matumaini makubwa ya urejeshwaji wa haraka wa mawasiliano hayo.
“Kasi ya ujenzi inaendelea kwa haraka sana pamoja na maji ya mvua kuwa mengi ninamatumaini itakamilika kwa wakati,” amesema Bi. Mkande.