News

TANROADS na ZANROADS waweka mikakati ya ushirikiano

TANROADS na ZANROADS waweka mikakati ya ushirikiano

 

Zanzibar

Januari 12, 2024

WAKUU wa taasisi za Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta na Wakala wa Barabara Zanzibar (ZANROADS), Mhandisi Cosmas Masolwa pamoja na Kamati ya Utekelezaji ya Hati ya Makubaliano ya mashirikiano wamekutana tarehe 12 Januari, 2024 baada ya sherehe za miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar kwa kuweka mikakati ya mashirikiano katika kikao kilichofanyika kwenye ofisi za ZANROADS eneo la Saateni.

 

Makubaliano ya awali 19 baadhi ni pamoja na kushirikiana katika masuala ya kiutendaji, utaratibu wa manunuzi, uendeshaji wa mizani, utoaji wa taarifa, matengenezo ya barabara, madaraja, na usalama barabani.

 

Mha. Besta amesema kikao hicho ni cha kwanza cha kutekeleza hati ya makubaliano yaliyofanyika Novemba 21, 2023 jijini Dodoma, katika kuanzisha mashirikiano baina ya taasisi hizi, ambayo yanalenga kuongeza uwezo na ufanisi, hususan katika eneo la wataalam kwa kuzingatia miongozo na kuweka ubora wa juu wa barabara za Tanzania Bara na Zanzibar.

 

Hatahivyo, amesema katika kikao hicho wamekubaliana kutengeneza mpango kazi wa utekelezaji, utakaotoa mwelekeo na dira ya utekelezaji wa makubaliano hayo.

 

“Huu ni mwendelezo tu lakini tutakuwa tunakutana mara kwa mara kama taasisi na tumeshaanzisha kwa kuunda timu ya utekelezaji yenye wataalam kutoka ZANROADS na TANROADS, na watakuwa wakikutana kwa kuangalia maeneo yote waliyokubaliana katika hati ya makubaliano,” amesema Mha. Besta.

 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya ZANROADS, Arch. Yasser de Costa amewashukuru TANROADS kwa kukubali kushiriki kwenye kikao hiki ambapo ametoa wito kwa pande zote mbili kuwa na mikakati, mipango kazi na ratiba maalumu, ili kuanza utekelezaji wa kazi husika.

 

“Tukubaliane kuwa kutia saini ni kitu kimoja na kutekeleza ni jambo muhimu sana hivyo tuwe na muda maalumu na kujua kazi zetu tunazitekeleza kwa namna gani, kuwa na uelewa mmoja kulingana wa kufanya majukumu yetu kwa ufasaha na hali ya juu,” amesema Arch. Costa.

 

Amesema TANROADS wanamipango mizuri ambayo wahandisi wa ZANROADS wanapaswa kujifunza kwa kupata elimu na ujuzi katika ujenzi na ukarabati wa barabara, na pia utengenezaji wa mashine ambazo nyingi ni mbovu na chakavu.

 

“Ninaamini kwa kushirikiana tunaweza kuzifufua na kuziendeleza mashine hizi ambazo hapa Unguja hadi Pemba ni mbovu, na zikaweza kufanya kazi tena na tukaweza kufanya kazi zetu ipasavyo,” amesema Arch. Costa.

 

Halikadhalika, amesema wamefarijika kukutana na wawakilishi wa Chuo cha Teknolojia ya Ujenzi cha Morogoro, ambao pia wameingia nao makubaliano ya kushirikiana katika utendaji kazi, ambapo sasa amewataka washirikiane pia na vyuo vya Sayansi na Teknoloji cha Karume na VETA Zanzibar, ili wanafunzi waweze kupata taaluma hizo na kwenda Bara kwa ajili ya kujiendeleza zaidi.

 

Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa ZANROADS Mha. Masolwa amesema mashirikiano hay ani mazuri kwa pande zote mbili.

 

“Wale waliozaliwa karibuni hawajui mashirikiano ya taasisi za Bara na Zanzibar, na haya nimazuri yanatuleta karibu na kuimarisha undugu wetu sisi ni nchi moja,” amesema Mha. Masolwa