News

SERIKALI KUJA NA 'MASTER PLAN' YA MIUNDOMBINU

SERIKALI KUJA NA 'MASTER PLAN' YA MIUNDOMBINU

 

10 Januari, 2024

Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi inaandaa Mpango Mkuu (Master Plan) wa Miundombinu ya nchi kulingana na mahitaji ya kiuchumi na kijamii itakayowezesha kurahisisha usafiri na usafrishaji kulingana na ongezeko la watu nchini.

 

Mpango huo utaangazia mtandao wa barabara wa nchi nzima kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) na Wakala ya Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA).

 

Hayo ameelezwa na Waziri wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa, tarehe 8 Januari, 2024 wakati alipokutana na Waziri wa Ardhi, Miundombinu, Usafiri na Utalii kutoka nchi ya Japan, Mhe. Konosuke Kokuba ambaye ameongozana na watalaamu mbalimbali wa Sekta ya Ujenzi kutoka nchini Japan.

 

"Miundombinu ya barabara inaenda sambamba na miundombinu mingine kama vile reli, kwa hivyo tutashirikiana na Wizara ya Uchukuzi kuandaa master plan ya miundombinu katika kuhudumia watanzania", amesema Waziri Bashungwa

 

Ameielekeza TANROADS kuandaa majadiliano ya Washauri elekezi na Wakandarasi kutoka Tanzania na nchi ya Japan ambao utakuwa endelevu ili kuendeleza mashirikiano ya karibu katika Sekta hiyo.

 

Aidha, Waziri Bashungwa amesema kuwa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshatoa maelekezo mahsusi ya kuweka mazingira wezeshi kwa Wakandarasi Wazawa ambapo Wizara imeanza kupitia mpango wa manunuzi ambao awali ulikuwa unawabana Makandarasi hao.

 

Katika mkutano huo, Waziri Bashungwa ameipongeza Serikali ya Japan kwa ushirikiano ambao wameendelea kuutoa tokea nchi ya Tanzania kupata Uhuru na ameendelea kuzialika Sekta Binafsi kutoka nchi hiyo kuendelea kufanya kazi kwa karibu zaidi na makampuni ya Tanzania, ili kubadilishana uzoefu.

 

Kwa upande wake, Waziri wa Ardhi, Miundombinu, Usafiri na Utalii kutoka Serikali ya Japan, Mhe. Konosuke Kokuba, amesema kuwa Serikali hiyo itaendelea kuimarisha mahusiano kati ya nchi hizo kwa kuendelea kujenga miundombinu yenye ubora katika miradi yote inayoendelea na ile ambayo inatarajiwa kutekelezwa.

 

Ameongeza kuwa kutokana ongezeko la watu katika nchi zinazokuwa zinahitaji teknolojia za kisasa katika ujenzi wa miundombinu nchini ili ziweze kutosheleza mahitaji.