BILIONI 60.1 KUKARABATI KIWANJA CHA NDEGE CHA SUMBAWANGA
Naibu Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya amesema zaidi ya shilingi bilioni 60.1 zinatarajiwa kutumika katika ukarabati na uboreshaji wa kiwanja cha ndege cha Sumbawanga.
Amesema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuimarisha usafiri wa anga nchini na kuwezesha maeneo mengi ya nchi kufikika kwa njia ya anga ambapo viwanja vinne vya Tabora, Kigoma, Sumbawanga na Shinyanga vinajengwa,
Akizungumza na wakazi wa Manispaa ya Sumbawanga Eng. Kasekenya amewataka kutoa ushirikiano kwa mkandarasi M/s Beijing Construction Engineering Group Co. Ltd ili akamilishe ujenzi huo kwa wakati.
“Tunatarajia ifikapo Machi 2025 kazi ya ukarabati na upanuzi wa kiwanja hiki katika njia ya kuruka na kutua ndege yenye urefu wa kilomita 1.750m, barabara za maungio na maegesho ya ndege, jengo la abiria, taa za kuongozea ndege na uzio wa usalama katika kiwanja hicho view vimekamilika”, amesema Eng. Kasekenya.
Amezungumzi umuhimu wa wakazi wa mkoa wa Rukwa kuhakikisha wanatumia fursa za uwepo wa miundombinu ya kisasa kujiletea maendeleo.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri huyo wa Ujenzi amekagua na kuelezea kuridhishwa kwake na kazi ya ujenzi wa barabara za Ntendo-Kizungu KM 25 ambayo ni sehemu ya barabara ya Ntendo-Muze-Kilyamatundu KM 179 na barabara ya Matai –Tatanda KM 25 ambayo ni sehemu ya barabara ya Matai-Kisesya KM 50 na kusisitiza kuwa nia ya Serikali ni kuzijenga barabara hizo zote kwa lami ili kuhuisha huduma za usafiri na uchukuzi na kuongeza biashara ya mazao katika ukanda wa Magharibi.
“Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatoa fedha nyingi kujenga barabara hizi, njia bora ya kumuunga mkono ni kuongeza uzalishaji wa mazao na kuilinda miundombinu hii kwa wivu mkubwa”, amesisitiza Naibu Waziri huyo.
Amewataka wakandarasi wote mkoani Rukwa kufanyakazi kwa kuzingatia muda, ubora na utabiri wa hali ya hewa ili kazi zisikwame na huduma za usafiri na uchukuzi zisisimame.
Naibu Waziri Kasekenya anaendelea na ziara yake ya kukagua ujenzi wa miundombinu katika kanda ya magharibi inayohusisha mikoa ya Tabora,Kigoma,Katavi na Rukwa.