News

TANROADS yaja na mkakati wa kuzuia ajali na uvamizi wa hifadhi za Barabara

TANROADS yaja na mikakati ya kuzuia ajali na uvamizi wa hifadhi za Barabara

 

01 Desemba, 2023

WAKALA ya Barabara Tanzania (TANROADS), wametoa mikakati madhubuti wa kuzuia ajali za kugongwa kwa waenda kwa miguu na uvamizi wa hifadhi za barabara kwenye maeneo mbalimbali hususan kwa mkoa Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa Mipango ya Miundombinu, Mhandisi Ephatar Mlavi amesema hayo wakati wa ziara ya mafunzo ya Wawakilishi wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar hivi karibuni, walipotembelea ujenzi wa miradi ya Daraja la Tanzanite lililopo eneo la Salender na barabara ya magari ya Mwendokasi Awamu ya Tatu inayojengwa kwa kuanzia eneo la Kamata hadi Gongolamboto.

Mhandisi. Mlavi amesema kuwa mikakati hiyo ni pamoja na kujenga njia za waenda kwa miguu pembeni mwa ilipojengwa barabara kuu na kuweka uzio unaowazuia kuingia barabarani.

Amesema mkakati mwingine ni pamoja na ujenzi wa madaraja ya vivuko vya waenda kwa miguu, ambavyo vinawaweka mbali kabisa na magari, ambayo yanawasababishia vifo au majeruhi ya kudumu wanapogongwa.

“Ajali chanzo chake sio barabara pekee lakini tumeendelea kutoa elimu kwa watumiaji wa barabara hizo, ili wasiendelee kupata madhara, ya kugongwa” amesema.

Katika hatua nyingine amesema hifadhi ya barabara inalindwa na Sheria ya Mwaka 2007 na Kanuni zake za mwaka 2009 zinazokataza mtu yeyote kufanya shughuli za kibinadamu kwenye hifadhi hizo za mita 30 kwa kila upande wa barabara na jumla kuwa mita 60.

Amesema bado TANROADS inaendelea kutoa elimu kwa umma juu ya matumizi ya hifadhi hizo, na kwa kupitia program za mameneja wa mikoa za kuwaondoa wavamizi.

“Pamoja na kwamba tunawaondoa lakini kunawakati tunawapa watu watumie kwa malipo kwa muda mfupi na kufanya kazi zisiozokuwa za kudumu kama vile kuweka bustani za maua au kupiga matofali ya kuuzwa, na mwananchi anakuwa akijiingizia kipato hadi eneo hilo litakapohitajika kwa kazi za uendelezaji,” amesema Mha. Mlavi.