News

Watumishi TANROADS wanolewa mfumo mpya wa utendaji kazi

Watumishi TANROADS wanolewa mfumo mpya wa utendaji kazi

 

30 Novemba, 2023

WATUMISHI wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Makao Makuu, wamenolewa kwa kupata mafunzo ya mfumo mpya wa utendaji kazi (PEPMIS na PIPMIS) yaliyofanyika tarehe 29 Novemba,2023 kwenye ukumbi wa Chuo cha Utalii mkoani Dar es Salaam.

Mmoja wa wawezeshaji wa mafunzo hayo, Afisa Utumishi Mkuu, Bw. Elibariki Funga kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, amesema wanatoa mafunzo haya kwa kuwa mfumo huu ni mpya unaotumia kielekroniki baada ya kuondolewa mfumo wa zamani uliokuwa ukitumia majadala magumu maarufu kama OPRAS. Mwezeshaji mwingine ni Abissay Ndaki kutoka OR.

Bw. Funga amesema mfumo huu utawafanya watumishi wa umma kuwajibika kwa kufanya kazi kwa ufanisi na tija, na pia kuhakikisha serikali inatoa huduma kama ilivyokusudiwa kwa wananchi

“Mafunzo haya yatafanyika nchi nzima kwa taasisi zote za serikali pamoja na wizara, ili kuwawezesha watumishi wa umma kuweza kuutumia kwa weledi, kwani umebeba dhamana zao katika kazi wanazofanya za kila siku kwa mwaka mzima, watakuwa wakipimwa na wasimamizi wao baada ya kupewa majukumu ya kufanya,” amesema Bw. Funga.

Naye Meneja Rasilimali Watu na Utawala wa TANROADS, Bw. Pilika Kasanda amesema mfumo huu umekuja wakati muafaka, ambapo watumishi wataweza kutekeleza majukumu yao waliyopanga kwa mwaka mzima, pamoja na kufanya tathmini yua utendaji wao kwa kipindi hicho.

Bw. Kasanda amesema mfumo huu utasaidia kuwawezesha wasimamizi wa kazi kuwasimamia watumishi bila upendeleo na manung’uniko, ambapo watumishi wataongeza ufanisi.

Kwa upande wa mmoja wa washiriki, ambaye pia ni Afisa Utawala Mwandamizi, Bi. Scolastica Mgaya kwanza ameipongeza serikali ya Awamu ya Sita iliyopo chini ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuruhusu mabadiliko katika mifumo ya kiutumishi, ili kuleta tija na ufanisi mahala pa kazi.

Bi Scolastica amesema mfumo huu wa kielekroniki ni mzuri kwa kuwa unaleta uwazi kwa kuwa ataonekana kuanzia ngazi ya msimamizi wake, Mtendaji Mkuu wa taasisi na mamlaka nyingine.

“Huu ni mfumo mzuri tofauti na iliyopita, mimi nimepita kwenye mifumo yote kuanzia ule wa siri, ukaja wa wazi (OPRAS) na sasa huu wa kielekroniki utaleta usimamizi mzuri wa utendaji wa watumishi wa umma,” amesema Bi. Scolastica