News

MTENDAJI MKUU WA WAKALA YA BARABARA TANZANIA (TANROADS) AIPONGEZA TANROADS SACCOS KWA KUPATA HATI SAFI NA KUONGEZA IDADI YA WANACHAMA 298 WAPYA KWA MIEZI TISA MWAKA 2023

MTENDAJI MKUU WA WAKALA YA BARABARA TANZANIA (TANROADS) AIPONGEZA TANROADS SACCOS KWA KUPATA HATI SAFI NA KUONGEZA IDADI YA WANACHAMA 298 WAPYA KWA MIEZI TISA MWAKA 2023

 

25 Novemba, 2023

MTENDAJI Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta amekipongeza chama cha Akiba na Mikopo cha watumishi wa wakala hiyo, TANROADS Saccos Limited kwa kuendelea kupata faida kubwa na kinajitosheleza kwa kuwa na fedha za  kutosha bila kuwa na madeni.

 

Amesema hayo katika hotuba yake, iliyosomwa na Meneja wa TANROADS Mkoa wa Dar es Salaam, John Mkumbo kwenye ufunguzi wa mkutano wa 10 wa Saccos hiyo uliofanyika tarehe 25 Novemba 2023 ukumbi wa NBAA jijini Dar es Salaam,

Ameeleza kufurahishwa na taarifa ya Mwenyekiti wa Bodi katika kipindi cha kuanzia  mwezi Januari hadi Septemba 2023, imeonesha kuwa chama kimepiga hatua kiuntendaji hususani katika ongezeko la wanachama, ongezeko la akiba, na mikopo.

Amewapongeza kwa kuwasilisha vitabu vya hesabu na kukaguliwa, hivyo kupata hati safi kwa miaka mitatu, hiyo ni kutokana na kuwa na mahesabu mazuri.

“Pamoja na changamoto mnazopata bado mmeweza kuwa na hati safi, hili ni jambo zuri sana,  nimeona jinsi mlivojipanga kwa kufuata taratibu ya kuita wajumbe wenu kwenye mkutano huu na akidi kwa kufuata sheria ya vyama vya Ushirika namba sita ya mwaka 2013 na kanuni zake za mwaka 2015 kifungu namba 46 kipengele cha kwanza na kifungu na 47 kipengele cha kwanza, pia sheria za nchi, sera na masharti na miongozo inayotolewa na Benki kuu (BOT) na Mamlaka zilizokasimiwa kushughulikia ushirika nchini” amesema.

 

Pia amewapongeza kutimiza matakwa ya kisheria ya kuitisha mkutano huu, ambao ndio dira, maono na mwelekeo wa chama hicho ambacho sasa kimetimiza miaka 17 tangu kuanzishwa.

Amesisitiza kuwa wamekuwa wakifanya jambo jema kwa kuijali jamii kwa kutoa misaada katika Mikoa mbalimbali kitu ambacho kinaleta matumaini hata kwa TANROADS.

Awali Mwenyekiti wa Bodi iliyomaliza muda wake, Bw. Augustino Konzo alisema katika kipindi cha mwezi Januari hadi Sept. 2023 chama kimepokea maombi ya wanachama wapya 298 na kufanya idadi ya wanachama wote kufikia 1355, hisa zilizopo ni 45,337 zenye thamani ya Tshs. 10,000 kwa kila hisa na kufanya thamani ya hisa zote kuwa tshs milioni 453.370 na akiba za wanachama zilizopo ni Bil. 594.263 na mikopo imetolewa kwa wanachama 569 ambayo ina thamani ya Tshs. Bil. 3.910.