News

MINISTER FOR WORKS HON. BASHUNGWA INAUGURATES TANROADS ADVISORY BOARD

Waziri wa Ujenzi Mhe. Innocent Bashungwa ameitaka Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kuandaa mkakati utakaowawezesha na kuwasaidia Wakandarasi Wazawa kukua na kutekeleza miradi mikubwa kama ambayo inatekelezwa na Wakandarasi wa Nje ili fedha watakayolipwa ibaki hapa Nchini kukuza uchumi wa Nchi yetu.

Pia ameitaka kutatua changamoto ya ongezeko la gharama za ujenzi wa miradi nje ya mikataba (Variation), na kushughulikia tatizo la rushwa kuanzia ngazi za awali za manunuzi, mikataba, utekelezaji, ufanisi na ubora wa viwango vya miradi.

Waziri Bashungwa ametoa maagizo hayo tarehe 04 Novemba 2023 Jijini Dodoma wakati akizindua bodi ya Ushauri ya Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) ambayo mwenyekiti wake anateuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mujibu wa sheria namba 13 ya Barabara ya mwaka 2007 kifungu 9 (2) (A-B).

Amesema " Asilimia 54 ya miradi inafanywa na Wakandarasi wazawa asilimia 46 Wakandarasi wa Nje, lakini ukiangalia kwenye asilimia unaona wazawa wana asilimia kubwa ukiipeleka kwenye namba unaona kuna tatizo, hii 46 % ya Wakandarasi wa nje hawazidi 500 lakini hii 54% ya wakandarasi wazawa ni zaidi ya 14,000 hivyo lazima tuwe na mkakati wa kuwasaidia wakandarasi wazawa bila kuathiri viwango vya majenzi''.

"Tarehe 21 mwezi huu wa novemba 2023 tumepanga kukutana na Wakandarasi Wazawa, Bodi hii nawaalika mje tukae nao, tujadili nao tuwasikilize baada ya hapo maazimio ya Mkutano yakatusaidie katika kazi na mipango yetu, ninamini bodi hii itatusaidie kusimamia hili vizuri'' amesisitiza Waziri Bashungwa.

Amesema ipo changamoto barabara ikiwa katika kipindi cha uangalizi muda mfupi baada ya Mkandarasi kukabidhi mradi unaharibika (Pre - Mature failure).

"Unakuta inatakiwa ikae miaka 20, mwaka wa tatu, wanne barabara imeanza kuharibika, naomba bodi hii ilipokee hili na kulifanyia kazi kwa uzito mkubwa sana, mkilisimamia hili vizuri tutaokoa mabilioni ya fedha za Watanzania, fedha ambazo tunazitumia kwenye matengenezo zitaweza kutumika kwenye mambo mengine ikiwemo kuendelea kuongeza mtandao wa Barabara Nchini na kujengwa kwa madaraja''.

"Lazima tupambane na changamoto ya rushwa na tuchukue hatua, mimi nitafurahi kusikia bodi mmefanya maazimio ya watumishi wachache ambao sio waadilifu mkaniletea kesi kwamba Waziri hatujasubiri Wizara mchukue hatua, kuna mtumishi huyu tumemkuta na changamoto moja mbili, tatu, achukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria za Utumishi wa Umma, nitafurahi sana ili tujenge timu ambayo itakuwa tayari kuwatumishia watanzania'" Amesisitiza.

Pia " Lazima tuweke uimara katika ufanyaji biashara na ujenzi wa viwanda katika Nchi yetu ili Dunia ije iwekeze na kuzalisha hapa, ndio maana Rais wetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anaendelea kuipa kipaumbele kikubwa sana Wizara yetu ya ujenzi kuhakikisha inapata bajeti na tunajenga barabara maeneo mbalimbali Nchini kwa Ma- trilioni ya fedha hivyo lazima tumsaidie kutafsiri maono na dhamira hiyo ili iweze kuwa fursa kwa Watanzania hasa vijana ambao tunajukumu la kuzalisha ajira ili waweze kuajiriwa''.

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi Balozi Mha. Aisha Amour amesema bodi hiyo inayoongozwa na Mwenyekiti Mhandisi Amin Nathaniel Mcharo aliyeteuliwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hasaan mnamo tarehe 13 June 2023; ina Wajumbe waziozidi 8 wanaoteuliwa na Mhe. Waziri wa Ujenzi kwa mujibu wa kifungu 9 (2) (B). cha sheria namba 13 ya Barabara ya mwaka 2007 ambapo wanatoka Taasisi mbalimbali ambazo ni Ofisi ya Rais TAMISEMI Mjumbe mmoja, Wizara ya Ujenzi, Bodi ya Mfuko wa Barabara (Roads Fund Board), Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wizara ya fedha, Bodi ya Utalii Tanzania, Mamlaka ya Uthibiti na Usafiri Ardhini pamoja na Shirikisho la Viwanda Tanzania.

Kwa Upande wake Mwenyekiti mpya wa Bodi hiyo, Mha. Amin Mcharo, ameahidi kutekeleza ipasavyo majukumu ya bodi ikiwa ni pamoja na kusimamia, kutathmini na kushauri kuhusu utendaji wa TANROADS ili kufikia malengo katika kutunza mtandao wa Barabara, viwanja vya ndege na kukuza maendeleo ya kijamii na kijamii ya Nchi yetu.

Ameongeza kuwa majukumu mengine ya bodi ni kuweka kipaumbele na malengo ya kiutendaji ya TANROADS, kuithinisha mipango kazi, kufuatilia utendaji, kudumisha uhusiano na mamlaka zingine za barabara ikiwemo TARURA, Kupitia taarifa na hesabu za mwaka na kuhakikisha kuwa wafanyakazi wa TANROADS wanafanya kazi kwa bidii na ueledi ili kufikia malengo yaliyopangwa.

Awali Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Mohamed Besta alisema TANROADS imejipanga na ipo tayari kufanya kazi kwa bidii, juhudi na maarifa kwa kushirikiana na bodi hiyo; ''pamoja na ukweli kwamba bodi hii ni mpya, ni ukweli pasipo shaka kuwa Wajumbe wa wake wanaifahamu vizuri TANROADS hivyo mipango na malengo yetu vitafanyika kama tulivyokusudia na hatmaye kufikia malengo yetu''.

Ameongeza kuwa pamoja na changamoto mbalimbali za kiutendaji zilizopo ndani ya Wakala wa Barabara Tanzania, lakini Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Wizara chini ya uongozi wa Waziri Mhe. Innocent Bashungwa inaendelea kuzifanyia kazi kwa karibu pengine kuzimaliza kabisa ndani ya kipindi cha muda mfupi na wakati; na kwamba TANROADS itahakikisha inafanya kazi kwa ufanisi na weledi wenye kuleta tija kuendana na thamani ya fedha zinazotolewa na kutumika kwenye miradi mbalimbali ya ujenzi.