News

TANROADS CHIEF EXECUTIVE, ENG. MOHAMED BESTA GUIDES EPC+FINANCING TEAM

Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania Mhandisi Mohamed Besta amesema TANROADS imepita katika vipindi tofauti lakini sasa ipo katika kipindi ambacho inabidi iwe na ubunifu wa kutumia mbinu mbalimbali na kutafuta namna bora zaidi ya kujenga barabara, na moja ya hatua ambazo zimechukuliwa na kuwekewa mkazo na Serikali ni pamoja na kutumia utaratibu wa EPC + F ili kujenga miundombinu hiyo kwa haraka zaidi.

Mhandisi Mohamed Besta amesema hayo leo tarehe 20, Agost 2023 Jijini Arusha alipotembelea eneo unapoanza mradi wa Ujenzi wa barabara ya Arusha - Kibaya - Kongwa wenye urefu wa kilometa 453.2 zinazojengwa kwa utaratibu wa EPC + F kwa gharama ya shilingi bilioni 546.294 ambazo ni fedha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa asilimia 100.

Akiwa ameambatana na timu ya Watalaamu wa barabara kutoka TANROADS Makao Makuu wakiongozwa na Meneja wa miradi ya PPP na EPC + F, Mhandisi Harold Kitainda na Meneja wa TANROADS mkoa wa Arusha Mhandisi Reginald R Massawe waliotembelea mradi huo, Mtendaji Mkuu wa TANROADS ameitaka timu hiyo ya Wataalamu kuangalia na kuisimamia miradi hiyo kikamilifu ili ijengwe kulingana na viwango vilivyowekwa, itekelezwe kwa muda uliopangwa na kuhakikisha inaendana na thamani ya fedha zilizotengwa kwa kila mradi husika.

"Kwa hatua tulizofikia hatuwezi kuendelea kutegemea njia zile zile za siku za nyuma kuendelea kujenga mtandao wetu wa barabara kwani tuna kilomita 36,760 kwa Nchi nzima, kati ya hizo 32.4% ni barabara kuu ambazo ni thelusi moja ya mtandao mzima, 67% bado haujafikiwa na barabara za lami, unaweza kuona ni kwa namna gani inabidi tubadilike na kuweza kujenga barabara kwa haraka zaidi" ameongeza Mha. Mohamed Besta.

Amesisitiza kuwa Serikali haitawaonea huruma Watendaji, Wakandarasi na watu wote wataohusika kukwamisha au kuhujumu utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo, ikiwemo ujenzi wa barabara zenye urefu wa jumla ya kilometa 2,035 zinazojengwa kwa kiwango cha lami sehemu mbalimbali Nchini kupitia utaratibu wa Engineering, Procurement plus Financing (EPC + F).

Mhandisi Besta ameongeza kuwa ili kufanikisha mradi huo kunategemea uwepo wa utekelezaji wa pamoja baina ya Wananchi, Watendaji, Wasimamizi wa mradi na Wakandarasi hivyo pale ambao Serikali inawekeza fedha takribani shilingi Trilioni 3.775 alafu kunatokea mtu au watu wahujumu, Serikali haitakuwa na huruma na badala yake itawachukulia hatua zinazostahili bila kujali nafasi ya mtu ili kuhakikisha kwamba tunalinda uwekezaji na rasilimali za Nchi.