News

KARATU TO MASWA 339 KM EPC+ FINANCING PROJECT

Serikali imeanza mchakato wa mradi wa ujenzi wa barabara ya Karatu - Mbulu - Hydom - Sibiti River - Lalago - Maswa yenye urefu wa Kilometa 339 kwa kiwango cha lami kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 553.493.

Mradi huo ni mmojawapo ya miradi 7 ya barabara ambayo utekelezaji wake ni kwa kutumia utaratibu wa Usanifu, Manunuzi, Ujenzi pamoja na Ufadhili, Engineering Procurement, Construction and Financing (EPC +F), mikataba ya miradi hiyo ilisainiwa tarehe 16 June mwaka huu 2023 jijini Dodoma na Mtendaji Mkuu wa Wakala ya barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Mohamed Besta kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akizungumza kwa nyakati tofauti na Wananchi wa maeneo unapopita mradi huo akiwa na timu ya watalaamu wanaotembelea mradi huo tarehe 18 Agosti, 2023, Meneja wa Miradi ya PPP na EPC + F Mhandisi Harold Kitainda amesema kwa ujumla barabara hiyo inapita katika Wilaya ya Karatu, mkoani Arusha, Mbulu mkoani Manyara, Mkalama Wilayani Singida na Wilaya za Meatu na Maswa mkoani Simiyu.

Amesema mradi huo ambao unagharamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa asilimia 100 unajengwa na Mkandarasi M/s China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) ikishirikiana na M/s China Railway 15 Bureau Group Corporation ambaye anatakiwa kukamilisha kazi hiyo ndani ya miezi 66.

Mhandisi Kitainda ameongeza kuwa Mradi huo unaotarajiwa kutengeneza zaidi ya ajira 1,000 unapita kwenye maeneo yenye shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwemo Kilimo, hasa cha mazao ya mahindi, vitunguu maji, mbaazi, vitunguu saumu, alizeti, ngano na ndizi, pia kuna shughuli za uvuvi na Ufugaji hasa wa ng'ombe, mbuzi, kondoo, kuku uchimbaji wa madini (Endagemu) pamoja na biashara ndogo ndogo kwenye maeneo ya vijiji.

Akizungumza mbele ya wananchi wa wilaya ya Maswa mkoani Simiyu Mkandarasi anayejenga mradi huo aliyekitambulisha kwa jina moja la Fu amesema kwa sasa wanafanya kazi ya usanifu na kuangalia sehemu nzuri ya kuweka kambi ya kuweka vifaa na Ofisi na kwamba. Watahakikisha wanaijenga barabara kwa ubora na kukamilisha kazi hiyo kwa wakati.