News

TANROADS STRATEGICALLY PLANS TO EXECUTIVE EPC + FINANCING PROJECTS

Meneja wa Miradi ya Public Private Partinerships- PPP na Engineering, Procurement, Construction and Financing (EPC +F) Mhandisi Harold Kitainda amewahakikishia Watanzania kwamba Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imejipanga kikamilifu kusimamia ipasavyo utekelezaji wa miradi ya barabara za lami zenye jumla ya kilometa 2,035 zinazojengwa kwa wakati mmoja hapa Nchini kwa kutumia utaratibu mpya wa EPC + F ikiwemo mradi wa kilometa 384 kutoka Handeni mpaka Singida.

Lengo ni kuhakikisha hakuna Mkandarasi anayekwenda kinyume na makubaliano ya mkataba, barabara zote zinajengwa kwa ubora na viwango vinavyokubalika kwendana na thamani ya fedha inayotolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kufanikisha miradi hiyo.

Mhandisi Kitainda ametoa kauli hiyo tarehe 16 Agosti, 2023 Wilayani Chemba mkoani Dodoma akiwa na timu ya wataalamu wa barabara kutoka TANROADS Makao Makuu ambao wanatembelea maeneo unapotekelezwa mradi wa ujenzi wa barabara ya Handeni - Kiberashi - Kijingu - Kibaya - Njoro - Olboroti - Mrijo Chini - Dalai- Bicha - Chambolo - Chemba - Kwa Mtoro - Singida yenye urefu wa Kilometa 384 kwa utaratibu wa EPC + F.

Amesema ujenzi wa barabara hiyo ambayo ni kiungo muhimu kati ya Mikoa ya Tanga, Manyara, Dodoma, na Singida unafanyika kwa wakati mmoja ambapo Utaratibu wa EPC + F umeainisha namna ya kumsimamia Mkandarasi ikiwa ni pamoja na kuweka Mwakilishi wa Mwajiri katika kila mradi pamoja na kuwa na timu ya Wataalamu ambayo inaweza kuangalia usanifu unafanywa na Wakandarasi ili kujiridhisha mradi una viwango ama la.

Amesisitiza kuwa ''tutatumia mitambo ya kisasa kukagua ubora wa mradi, kuhakikisha kazi inafanyika kama inavyotakiwa bila kucheleweshwa na kuhakikisha viashiria hatarishi anavibeba Mkandarasi bila kuwepo na visingizio vya usumbufu wa kucheleweshewa malipo wala kuchelewesha mradi".

"Kwenye utekelezaji wa miradi wa aina hii kama Mkandarasi hajafanya Usanifu vizuri na akatekeleza mradi ulio chini ya viwango atapata hasara kwa kurudia mradi kwa gharama zake mwenyewe, TANROADS na wataalamu wetu tumeweka jicho letu kufuatilia karibu kila hatua ya mradi husika, hivyo lazima Mkandarasi aongeze umakini katika ufanyaji kazi wake" ameongeza Mhandisi Kitainda.

Aidha Mradi huo wa EPC + F unapitia katika Wilaya ya Handeni mkoani Tanga; Kiteto mkoani Manyara; Kondoa na Chemba Mkoani Dodoma pamoja na Wilaya za Ikungi na Singida Mkoani Singida; katika vijiji vya: Kilegulu, Kwediboma, Kisangasa, Mgera, Nkoa, Kwamtawazi, Kiberashi na Ngaloni kwa mkoa wa Tanga; Kijungu, Kibaya, Njoro, Olboloti Mrijo Chini katika Mkoa wa Manyara; Mrijo Juu, Songolo, Chandama, Goima, Chemba, Donzee, Mombosee, Bubutole, Kwa Mtoro, Ovada Mkoani Dodoma pamoja na Kinyamshindo, Makiungu, na Kititimo.