News

EPC + FINANCE PROJECTS ARRANGEMENT IN TANGA REGION

Ujenzi wa mradi wa barabara ya Handeni - Kiberashi - Kijingu - Kibaya - Njoro - Olboroti - Mrijo Chini - Dalai - Bicha - Chambolo - Chemba - Kwa Mtoro - Singida yenye urefu wa Kilometa 389 unaotarajiwa kuanza hivi karibuni kwa kiwango cha lami umetajwa kuwa na manufaa makubwa kwa wakazi wa mkoa wa Tanga, Manyara, Dodoma, Singida na maeneo ya Jirani ikiwemo kutoa ajira zaidi ya 1000 kwa wazawa, kuondoa adha ya usafiri na usafirishaji na hivyo kuchochea shughuli kiuchumi na maendeleo.

Ujenzi wa barabara hiyo unatekelezwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) kwa kutumia utaratibu wa Engineering, Procurement, Construction and Financing (EPC +F) ambao ni dhana inayohusisha utekelezaji wa mkataba wa Ujenzi baina ya Mkandarasi na Taasisi ya Umma inayotekeleza mradi, ambapo katika utaratibu huo Mkandarasi anatoa taarifa ya vyanzo vya mikopo kwa ajili ya kugharamia utekelezaji wa mradi husika hivyo mkandarasi hatoi fedha bali anakuwa ni kiunganishi kati ya watoa fedha na (lender's) na Mkopaji (Borrower).

Mwakilishi wa Meneja wa TANROADS mkoa wa Tanga Mhandisi Zuhura Amani amebainisha hayo tarehe 15 Agosti, 2023 alipokuwa akizungumza na timu ya wataalamu kutoka TANROADS Makao Makuu ikiongozwa na Meneja wa miradi ya Public Private Partinerships- PPP na Engineering, Procurement, Construction and Financing (EPC +F) Mhandisi Harold Kitainda walipotembelea eneo la mradi huo Wilayani Handeni kwa lengo kujenga uelewa na kuitengeneza mikakati mahususi kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa ujenzi wa barabara hiyo.

''Sisi tunashukuru sana kuletwa kwa mradi huu kwenye Mkoa wetu kwa sababu barabara hii ni muhimu sana, magari makubwa na mazito yanapita eneo hilo, kuna shughuli mbalimbali zinafanyika katika mkoa huu, mbali na kilimo kuna machimbo mbalimbali ya madini ikwemo Graphite pamoja na machimbo madogo madogo ya dhahabu ambayo yanafanywa na Wachimbaji wadogo wadogo, barabara hii itakapokamilika pia itawasaidia watumiaji wanaotoa mizigo Bandari ya Tanga kupunguza muda wa safari na kuitumia kama barabara fupi kuelekea katika mikoa ya Jirani badala ya kutumia barabara ya Morogoro ambayo inapita Segera kwenda mikoa ya Kaskazini'' Ameeleza Mhandisi Zuhura Amani.

Ameongeza kuwa ''Barabara ya Morogoro sasa hivi imezidiwa kwa hiyo, hii barabara itakwenda kupunguza uzito wa magari kwenye barabara ile na baadae itatusaidia kupunguza hata gharama za kufanya matengenezo ya mara kwa mara, kwani mzigo unapokuwa mzito, barabara huwa zinaharibika kwa kasi sana, uwepo wa barabara nyingi utasaidia kumaliza tatizo hilo na vile vile zitasaidia watu kufikiwa kwa wakati na hivyo kukuza uchumi wa mkoa wa Tanga na Nchi kwa Ujumla''.

Akizungumza kwa niaba ya mkandarasi anayejenga mradi huo kwa gharama ya Shilingi bilioni 432 kwa kutumia utaratibu wa EPC +F kutoka kampuni ya China Railway Construction Engineering Group, Mhandisi Zhang Tao ameahidi kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati ndani ya miezi 36 iliyokubaliwa kwenye mkataba ukiwa na viwango vinavyokubalika na kuendana huku akiomba Viongozi na Wananchi wa maeneo husika kumpa ushirikiano katika kipindi chote cha utekelezaji wa mradi huo.