Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameipongeza Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kupitia TANROADS kwa kufanya kazi kubwa ya kufanikisha maonesho ya Sabasaba Mwaka 2023 kwa kujenga barabara nzuri za kiwango cha lami ndani vya Viwanja vya Sabasaba Jijini Dar es Salaam na kuongeza hadhi na muonekano mzuri wa viwanja hivyo.
Waziri Mkuu Mhe. Majaliwa ametoa kauli hiyo leo Jumatano tarehe 05 Julai 2023 alipomwakilisha Mheshimiwa Dkt. Rais Samia Suluhu Hassan kwenye ufunguzi wa maonesho ya biashara ya kimataifa ya 47, yanayoendelea katika viwanja vya Sabasaba Temeke jijini Dar es Salaam.
"Hongereni sana TANROADS kwa kazi hii,
Mtendaji Mkuu na Meneja wa Dar es Salaam mmenisikia kwa niaba ya Serikali nawapongeza sana, natamani mwakani tukija tukute barabara zote za vumbi hapa ziwe zimewekwa lami, napenda kuwahakikishia kwamba Serikali itaendelea kushirikiana nanyi katika shughuli zote za Maendeleo'' Ameongeza Waziri Mkuu.
Wakati huo huo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameikabidhi Wakala ya Barabara Tanzania TANROADS tuzo maalum ya Mchango Mkubwa walioutoa katika kufanikisha maonesho hayo, tuzo ambayo imepokelewa na Mtendaji Mkuu wa TANROADS Mhandishi Mohamed Besta.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade Bi.Latifa Khamis amesema ''TANROADS wametujengea barabara zetu kwa kutumia (CSR) (Corporate Social Responsibility), Wajibu wa Shirika kwa Jamii katika kuhakikisha maonesho yetu yanaleta fursa za Kimataifa, huku Mwenyekiti wa bodi ya Tantrade Prof. Ulingeta Mbamba akisema juhudi za TANROADS katika kujenga barabara hizo zimepandisha hadhi uwanja huo wa maonesho hivyo kutoa hamasa kwa washiriki.
Akizungumza muda mfupi baada ya kupokea tuzo hiyo ya pongezi Mtendaji Mkuu wa TANROADS Mhandisi Mohamed Besta amesema TANROADS inashirikiana na taasisi nyingine katika kuleta maendeleo na kuimarisha miundombinu.
Ameongeza kuwa ''kushirikiana na wenzetu wa Tantrade kuhakikisha miundombinu ndani ya uwanja wa maonesho inaimarika zaidi, kutokana na maelekezo aliyoyatoa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa tutaendelea kushirikiana kuhakikisha mwaka ujao tunaboresha zaidi miundombinu hii''
Naye Msimamizi wa Kitengo cha Matengenezo TANROADS Mkoa wa Dar es Salaam Mhandisi Eliseus Mtenga amesema kazi ambazo zimefanyika kwenye uwanja huo ni pamoja na ujenzi na matengenezo haraka ya barabara kwa kuziba maeneo yaliyokuwa mabovu na kuweka tabaka la lami zito jipya km 1.85, aliyefanya kazi hiyo ni mkandarasi mzalendo kutoka kampuni ya Naki Construction Co. Limited kwa gharama ya shilingi milioni 746.