Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi imeomba kuidhinishiwa jumla ya Shilingi Trilioni 3.554, katika mwaka wa fedha 2023/2024, kati ya fedha hizo, Shilingi Trilioni 1.468. ni kwa ajili ya Sekta ya Ujenzi na Shilingi Trilioni 2.086, ni kwa ajili ya Sekta ya Uchukuzi.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa ameomba fedha hizo mapema leo Tarehe 22 Mei -2022 wakati akisoma Bajeti ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya wizara hiyo Bungeni Mjini Dodoma.
Kuhusu Miundombinu Waziri Prof. Mbarawa amesema serikali kupitia TANROADS inatarajia kuanza ujenzi wa miradi saba (7) ya barabara yenye jumla ya kilometa 2,035 kwa kutumia utaratibu wa Engineeering Procurement Construction and Finance ( EPC + F) na kuanza utekelezaji wa ujenzi wa barabara kutoka Kibaha – Chalinze – Morogoro Expressway yenye urefu wa kilometa 205 kwa kutumia utaratibu wa kushirikisha Sekta Binafsi (Public Private Partnership – PPP.
Amesema pia unaendelea na ujenzi wa miradi mikubwa ya barabara katika maeneo mbalimbali yenye jumla ya urefu wa kilometa 1,031.98 na Ujenzi wa Barabara iliyosaniwa Katika Mwaka wa Fedha 2022/23 yenye jumla ya urefu wa kilometa 393.6
Amesisitiza kuwa miradi yote ya barabara na madaraja ikamilika itakuwa na jumla ya km 3,934.7 za barabara zilizojengwa kwa lami ambazo zitaongeza urefu wa mtandao wa barabara za lami zilizopo sasa za km 11,587.82 na kufikia km 15,522.52 ambalo ni sawa na ongezeko la 34%.
Waziri Prof. Mbarawa ameongeza kuwa Serikali inaendelea na utekelezaji wa mradi ujenzi wa uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Msalato Dodoma pamoja na Kuendelea na kazi za ukarabati na upanuzi wa viwanja vingine vya ndege katika mikoa mbalimbali ikiwemo Kiwanja cha Ndege cha Songwe, ukarabati na upanuzi wa Viwanja vya Ndege vya Sumbawanga, Shinyanga, Tabora na Kigoma.