News

UJENZI WA BARABARA YA NJIA NNE MBEYA WAANZA

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa ametaka usimamizi madhubuti wa Ujenzi wa Barabara ya Igawa - Songwe – Tunduma, Sehemu ya
3, Ujenzi wa Njia Nne kutoka Nsalaga (Uyole) mpaka Ifisi (Kiwanja cha Ndege cha Songwe) yenye urefu wa kilometa 29.

Profesa Mbarawa ametoa maelekezo hayo wakati wa hafla ya Utiaji Saini Mkataba wa Ujenzi wa Barabara ya Igawa - Songwe – Tunduma, Sehemu ya 3, Ujenzi wa Njia Nne kutoka Nsalaga (Uyole) mpaka Ifisi (Kiwanja cha Ndege cha Songwe) yenye urefu wa kilometa 29, makubaliano ambayo yamefanyika mkoani Mbeya.

Akizungumza mara baada ya kushuhudia makubaliano hayo Prof. Mbarawa amesema barabara hiyo inajengwa na serikali kwa asilimia 100 ni lazima isimamiwe ipasavyo ili iende sawa na thamani ya fedha inayotolewa kwa jasho la wananchi chini ya serikali ya awamu ya sita.

Amesema Barabara hiyo itaimarisha usafirishaji wa abiria na bidhaa mbalimbali ikiwemo bidhaa za mazao ya chakula na biashara, mazao ya misitu, na mizigo ya aina mbalimbali pamoja na kuimarisha shughuli za kijamii kwa ujumla.

Ameongeza kuwa Barabara hii ni kiungo muhimu katika nchi za Afrika Mashariki na nchi za Kusini mwa Afrika lakini pia itarahisisha usafirishaji wa bidhaa katika nchi za
Malawi, Zambia na Kongo zinazokwenda na zinazotoka bandari ya Dar es Salaam.

Katika hatua nyingine Waziri Mbarawa amesema serikali iko katika mchakato mbalimbali ya ujenzi wa barabara za mkoa huo ambapo takribani km 420 zinatarajiwa kujengwa, Mkoani humo.


Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania Mhandisi Rogatus Mativila amesema barabara hiyo ambayo ilifanyiwa ukarabati miaka 30 iliyopita itajengwa kwa kifusi cha changarawe kilichochanganywa na saruji (C2) lenye unene wa milimeta 350 ikiwa ni tabaka la chini la msingi (Sub-Base) na tabaka la juu la msingi litajengwa kwa kutumia zege la lami (Asphalt Concrete Base) lenye unene wa milimeta 210, huku ikiwa na Upana wa barabara wa mita 7.0 kwa kila barabara ya njia mbili ya upande mmoja, upana wa mita 9.0 kwa sehemu ya katikati ya kutenganisha barabara (Median) na kutakuwa na njia za waenda kwa miguu (pedestrian walkways) yenye upana wa mita mbili na nusu (2.5) kila upande.


Barabara hii inayojulikana kama TANZAM Highway na inapita katika mbuga za wanyama za Mikumi National Park, inahusisha Mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Iringa,
Njombe, Mbeya na Songwe.