News

GOVERNMENT SIGNS CONTRACT FOR MORE PAVED ROADS IN KIGOMA

BARABARA ZA LAMI KIGOMA KUONGEZEKA

 

WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amewataka wananchi wa Mkoa wa Kigoma kutumia fursa ya ujenzi wa miundombinu ikiwemo barabara za lami kufanyakazi kwa bidii na kukuza uchumi.

 

Amesema ujenzi wa barabara za lami, meli katika ziwa Tanganyika, reli ya kisasa (SGR) na uboreshaji wa uwanja wa ndege ni dhamira ya Serikali katika kuunganisha mkoa huo na nchi jirani.

 

 

Amesema Takriban kilometa 400 za lami zinajengwa Kigoma ikiwa ni lengo la Serikali ya awamu ya sita  kuhakikisha huduma za usafiri na uchukuzi kwa nyanja zote zinaimarika nchini kote ili kuibua fursa zote za uchumi ikiwemo kilimo na biashara.

 

 

 

Akishuhudia utiaji saini mkataba wa ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Kibondo – Mabamba yenye kilometa 47.9, Waziri huyo wa Ujenzi amewahakikishia wakazi wote watakaoguswa na mradi huo kulipwa fidia kwa mujibu wa sheria.

 

 

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Eng. Rogatus Mativila amesema barabara hiyo ya Kibondo - Mabamba yenye urefu wa kilometa 47.9 inaunganisha mkoa wa Kigoma na mikoa ya Kagera, Geita na nchi ya Burundi kupitia Gieta hivyo kukamilika kwake kwa lami kutachochea biashara katika ukanda wa magharibi.

 

 

Amesema mkandarasi aliyeshinda ujenzi wa barabara hiyo ni kampuni ya CHICO kutoka China na ujenzi wake utatumia miezi 24 ambapo  takriban  shilingi bilioni 63.7 zitatumika.