News

PIC YARIDHISHWA NA UTENDAJI WA TANROADS

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma(PIC), imeipongeza Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) kwa kazi kubwa ya utekelezaji wa ujenzi wa miradi mbalimbali ya miundombinu nchini.

Akizungumza kwa niaba ya kamati hiyo, Mwenyekiti wa Kamati, Mhe.Jerry Slaa, alisema TANROADS imeendelea kufanya kazi kubwa kwa taifa ya ujenzi wa miundombinu na kamati ya PIC inawapongeza, lakini akasisitiza kuwa TANROADS  imepewa dhamana kubwa na  Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kufanya kazi kwa bidii zaidi.

''Tunawapongeza sana kwa kazi kubwa, sisi ni Kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma, tumekuja kwa ajili ya kupata taarifa ya mradi wa ujenzi wa miundombinu ya mabasi yaendayo haraka (Awamu ya Pili), ambao umekuwa unasuasua kukamilika,'' alisema.

Aidha, Kamati iliitaka TANROADS, kumsimamia kwa ukamilifu mkandarasi anayejenga miundombinu ya barabara ya mabasi yaendayo haraka ( Awamu ya Pili) kutoka Gerezani hadi Mbagala ili kuhakikisha Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, inatekeleza azma yake ya kufanya kazi kwa kasi kubwa katika kukamilisha miradi.

Alisema mradi huo ni muhimu na ndio maana Rais Samia alitoa maagizo ya kutaka mradi kumalizika kwa haraka ili wananchi wanufaike na mradi huo, ambao kumalizika kwake utakuwa na faida kubwa.

"TANROADS mnafanya kazi nzuri lakini mwenendo wa makandarasi sio mzuri, mnapaswa kumfuatilia kwa karibu ili amalize mradi huu kwa wakati na kwa ufanisi mkubwa, kwakuwa kuchelewa kwake kunasababisha sintofahamu kwa wananchi," alisema Mhe. Slaa.

Kwa upande wake, Mjumbe wa kamati hiyo, Mhe. Augustine Vuma, naye aliitaka TANROADS kuhakikisha wanawasimamia wakandarasi mbalimbali nchini na kuwachukulia hatua wale wanaochelewesha utekelezaji wa miradi mbalimbali.

Akitoa taarifa ya maendeleo ya  mradi mbele ya kamati, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Rogatus Mativila, alisema mradi wa Ujenzi wa Miundombinu ya Mabasi yaendayo Haraka ( Awamu ya pili) hadi sasa umefikia asilimia 50.7 kwa upande wa ujenzi wa miundombinu ya barabara, ambayo ilikuwa ni ‘Lot 1’.

Alisema katika mradi huo, kazi za ujenzi wa majengo ikiwemo karakana 1, vituo vikuu 2 na vituo mlisho vinne vimeshakamilika tangu Julai 31, 2021 na sasa sehemu hiyo iko katika muda wa uangalizi wa mwaka mmoja kama mkataba unavyotaka.

''Tunatarajia mwakani kuumaliza mradi huu, ambapo TANROADS imeshakaa na mkandarasi na kuzungumza naye, ambaye kuchelewa kwake kulitokana na matatizo ya Uviko-19, hivyo Machi 27, 2023 mradi huu utakamilika'' alisema.

Wakati huo huo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ( Ujenzi), Ludovick Nduhiye, alisema ushauri wote uliotolewa na Kamati ya Bunge kupitia kwa kamati hiyo utafanyiwa kazi ikiwemo kuusimamia mradi hadi kukamilika kwa wakati.