News

TANROADS YAKAMILISHA KUUNGANISHA DARAJA JIPYA LA SELANDER

Mradi wa ujenzi wa Daraja jipya la Selander unaosimamiwa na Serikali kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), umefikia asilimia 93, huku Desemba mwaka huu ukitarajiwa kuanza kutumika.

Akizungumza baada ya kukagua na kushiriki uwekaji wa zege kuunganisha kipande cha mwisho cha daraja, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Rogatus Mativila amesema mradi wa daraja jipya la selander upo katika hatua za mwisho za ukamilishaji.

Ameeleza mwezi Desemba mwaka huu, Daraja litaanza kutumiwa na magari pamoja na waenda kwa miguu.

Akifafanua baadhi ya faida za mradi , Mhandisi Mativila, amesema changamoto ya msongamano wa magari inayolikabili daraja la awali katika barabara ya Ali Hassan Mwinyi, itakuwa historia.

“Ule msongamano mkubwa uliokuwa ukilikabili daraja dogo la zamani la Selander hautakuwepo tena, kwa sababu daraja hili jipya litatumika pamoja na la zamani,” amesema.

Amefafanua kwamba, mbali na kupunguza msongamano, uzuri wa daraja jipya la Selander utakuwa kivutio cha utalii, hata mgeni akitoka mbali atatamani kwenda kuliona daraja hilo.

Hata hivyo, Mhandisi Mativila amesema kwa sasa wanafanya mawasiliano na Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) Wilayani ya Kinondoni ili kuendeleza kuboresha barabara zao kutokea Coco Beach kwenda SeaCliff Hotel hadi Slip Way.

“Katika barabara tunazounganisha kuna hii ambayo tumejenga ambayo inaishia Coco Beach, lakini tunawasiliana na wenzetu wa TARURA Kinondoni, ili waboreshe barabara zao kutoka Coco kwenda Sea Cliff izunguke kuja Slip Way ili watu wanaokwepa msongamano wawe na namna ya kupita hadi kutokea nje ya Jiji au kuingia,” ameeleza Mhandisi Mativila.

Mradi wa Daraja jipya la Selander unatekelezwa na Kampuni ya Uhandisi ya GS Engineering kutoka Korea Kusini, Mhandisi Mshauri ni Kampuni ya Yooshin Engineering kutoka Korea Kusini ikishirikiana na Afrisa Consulting ya Tanzania.

Aidha, mradi unatekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 243 ambazo ni mkopo wa masharti nafuu kutoka serikali ya Korea na fedha za serikali ya Tanzania.