News

NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI MHE. MWITA WAITARA AKUTANA NA UONGOZI WA TANROADS

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Mwita Waitara amefanya Kikao Kazi na Uongozi wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) katika Makao Makuu ya TANROADS Agosti 27, 2021 Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika Mkutano huo kwa njia ya mtandao na Mameneja wa TANROADS wa Mikoa, Mhe. Naibu Waziri alisema lengo la kikao hicho ni kuongea na Mameneja wa Mikoa kuhusiana na changamoto mbalimbali zinazojitokeza  hususan kutoka kwa wasafirishaji juu ya baadhi ya  vituo vya Mizani na kuzipatia ufumbuzi kwa wakati.

Mhe. Waitara alieleza Menejimenti  kwamba wana jukumu la kuisaidia Serikali katika kuhakikisha mahusiano mazuri yanakuwepo baina ya Wafanyabiashara nchini hasa Wasafirishaji kwani sekta hiyo ni kichocheo cha uchumi wa nchi.

Alisisitiza suala la uelimishaji wasafirishaji juu ya shughuli za mizani ili kuepuka changamoto mbalimbali zinazojitokeza na malalamiko yaliyopo hususan juu ya  faini wanazotozwa wasafirishaji huku baadhi ya mizani kuwa na changamoto za kiufundi.

Aidha, aliuagiza Uongozi wa TANROADS kuwa na utaratibu wa kubadilisha watumishi katika maeneo ya Mizani mara kwa mara ili kuongeza ufanisi katika vituo hivyo.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Matengenezo Eng. Vincent Tarmo, alimuahidi Mhe. Naibu Waziri kufanyia kazi maagizo hayo na kuwataka wasafirishaji kuwasiliana na TANROADS katika Mikoa husika kwa haraka iwapo watakutana na changamoto zozote.

Akizungumza katika kikao hicho, Kaimu Mtendaji Mkuu wa TANROADS Eng. Ephrem Kirenga alimuahidi Naibu Waziri kuyafanyia kazi maagizo yote aliyoyatoa katika kikao hiki muhimu.