News

FIDIA YA WANANCHI WA DODOMA JIJI WANAOPISHA UJENZI WA UWANJA WA NDEGE MSALATO NA BARABARA YA MZUNGUKO

 

Fidia ya wananchi wa maeneo wanaopisha ujenzi wa kiwanja cha kimataifa cha Ndege cha Msalato na Barabara ya mzunguko imekamilika na itaanza kutolewa ndani ya muda wa wiki mbili zijazo.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mh. Dr. Leonard Chamuriho wakati wa ziara ya kukagua  utekelezaji wa miradi ya uwanja wa ndege Msalato na barabara ya mzunguko.

“Tumekamilisha taratibu zote za malipo ya fidia ya takribani Tsh 14 bilioni kwa wananchi wote wanaopisha ujenzi wa uwanja wa Ndege Msalato na wanaopisha barabara ya mzunguko,hivyo muda sio mrefu tutawafikia na kuwalipa fedha wananchi wote waliopitiwa na miradi hii mikubwa”Alisema Dr.Chamuriho

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Mh. Seleman Kakoso ameitaka Serikali kuhakikisha wananchi wote wanalipwa mapema ili kuruhusu utekekelezaji wa miradi hii mikubwa inayogharimu zaidi ya Trilioni 1 kwa ujumla wake na kuitaka Wizara kuwasimamia wakandarasi vizuri ili miradi yote ikamilike kwa muda uliopangwa.

Akitoa shukrani zake,Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Mh Anthony Mavunde ameishukuru Serikali kwa kukamilisha taratibu zote za malipo ya fidia kwa wananchi ambao wamesubiri kwa muda mrefu na kuitaka serikali kuzingatia taratibu zote za kisheria za malipo ya fidia ili kila mwananchi apate haki yake stahili.

Mbunge Mavunde pia ameishukuru serikali kwa kutenga kiasi cha **Bilioni 16 **ambazo zitajenga vituo vya Afya,Visima virefu vya maji na Gari la kubeba wagonjwa kwa maeneo yote miradi hii ya barabara inapotekelezwa