News

‘Daraja la TANZANITE kudumu zaidi ya miaka 100’

Na Mwandishi Wetu

MHANDISI Miradi wa Daraja jipya la Selander (TANZANITE) Mhandisi Rajab Manger, amesema mradi wa Daraja jipya la Selander umeanza utekelezaji wake baada ya  Serikali kuona changamoto kubwa ya foleni za magari katika barabara ya Ali Hassan Mwinyi na Barack Obama Jijini Dar es Salaam.

Amesema kutokana na changamoto ya daraja la zamani kuzidiwa na magari, Serikali ilianza mpango wa kujenga daraja lingine ambalo litasaidiana na miundombinu mingine ili kuondoa kero ya foleni katika Jiji la Dar es Salaam.

Mhandisi Manger, amezungumza hayo hivi karibuni, katika eneo la daraja jipya la Selander (TANZANITE ) jijini Dar es Salaam,  na kuanisha kwamba daraja hilo likimalizika litasaidia kuondoa foleni katika barabara ya Ali Hassan Mwinyi na Barack Obama eneo la daraja la zamani la Selander.

Amesema mradi wa daraja jipya la Selander (TANZANITE ) ulianza mwaka 2018, ambapo kazi ya usanifu ilikuwa imekamilika na kazi zilianza kwa kuchimba msingi ambapo nguzo zaidi ya 200 zimeingia chini ya bahari.

Mhandisi Manger amesema kuwa, mradi  huu wa daraja  la TANZANITE utapunguza kero ya foleni jijini Dar es Salaam na utasaidia kukuza sekta ya utalii kwasababu eneo hilo liko pembeni ya fukwe ya bahari ambapo watu wengi watakuwa wakienda kuvinjari.

Amesema daraja la zamani la Selander linapitisha takriban magari zaidi ya 45,000 kwa siku, hivyo litakapokamilika daraja hili jipya TANZANITE litasaidia sana kupunguza idadi ya magari yanayopita katika daraja la zamani la Selander na hivyo kuepusha kabisa msongamano wa foleni.

“Gharama za mradi huu wa Daraja la Tanzanite ni takribani shilingi bilioni 243, na unasimamiwa na Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS),  na Mkandarasi wa mradi wa huu ni GS Engineering kutoka Korea Kusini, Mhandisi Mshauri ni Kampuni ya Yooshin Engineering kutoka Korea Kusini ikishirikiana na Afrisa Consulting ya Tanzania.’ Alisema Eng. Manger.

Daraja hili lenye urefu wa kilometa 1.03 litakuwa na njia nne za magari na njia mbili za watembea kwa miguu, litajengwa pamoja na barabara unganishi zenye jumla ya kilometa 5.2.

Mhandisi Manger amesema daraja la TANZANITE litakuwa la kipekee, kitaalamu ni extra dosed ukilinganisha na madaraja ya nchi nyingine, kwa hapa nchini litakuwa la pili kwa urefu likitanguliwa na la JP Magufuli Bridge (Kigongo-Busisi).

“Pamoja na kuleta faida nyingi, mradi huu umeweza kutoa ajira kwa watu wetu na kupata kipato cha kuendesha maisha yao, hivyo tunaishukuru Serikali kwa kuleta miradi kama hii inayosaidia wananchi kupata kipato,” amesema Mhandisi Manger.

“Ujenzi kama huu unagharimu pesa nyingi sana, pesa ambayo ni yetu sote, kwa hiyo ni wajibu wetu kuweza kuitunza  miundombinu hii kwa ajili yetu na hata vitukuu vyetu vitaweza kulitumia daraja hili ambalo litadumu zaidi ya miaka 100,” amesema Mhandisi Manger.