News

BARABARA YA MBULU - HYDOM KUJENGWA KWA KIWANGO CHA LAMI - NAIBU WAZIRI UJENZI NA UCHUKUZI

BARABARA YA MBULU- HYDOM KUJENGWA KWA KIWANGO CHA LAMI-  NAIBU WAZIRI  UJENZI INA UCHUKUZI

Na Mwandishi wetu.

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Msongwe Kasekenya amesema barabara ya Mbulu-Hydom yenye urefu wa kilomita 70.5 ni sehemu ya barabara ya Karatu, Mbulu-Hydom, Sibiti, Lalago, Maswa zenye urefu wa kilomita 398 zinahudumiwa na Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS).

Mhandisi Kasekenya ameeleza hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Mbulu Mjini, Zacharia Paul Isaay lBungeni jijini Dodoma kuhusu ujenzi wa barabara  ya Mbulu-Hydom,   amesema kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa awali wa barabara hiyo kupitia mradi wa Serengeti (Southern Bypass), ili kuijenga kwa kiwango cha lami umekamilika.

Naibu Waziri amesema kazi hiyo imefanywa na kampuni ya HB Golf Engineer na KGGB zote za Ujerumani mwaka 2016 kwa ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KFW).

Amesema kwa kuzingatia umuhimu wa barabara hiyo, Serikali ilianza kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa sehemu ya Mbulu-Hydom yenye urefu wa kilomita 50 kwa kiwango cha lami, ambapo katika mwaka wa fedha 2019/2020 ilitenga shilingi bilioni 1.45 na mwaka huu wa fedha imetenga shilingi bilioni 5.

Naibu Waziri amesema ujenzi wa barabara hiyo utatekelezwa kwa njia ya kisanifu na zabuni ya kazi hiyo itatangazwa wakati wowote katika wakati huu wa mwaka wa fedha.

Katika mwaka wa fedha wa 2020/2021, zimetengwa shilingi milioni 401 kwa ajili ya kuifanyia matengenezo mbalimbali barabara hiyo ili iendelee kupitika katika majira yote ya mwaka huu.