Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imepongezwa kwa kuwezesha utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Daraja la Pangani mkoani Tanga, ambao umefikia asilimia 72, huku kazi zikiendelea katika hatua ya ujenzi wa sehemu ya juu ya daraja hilo.
Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Tanga, Mhandisi Msama Kosani Msama, amesema mradi huo unahusisha ujenzi wa Daraja la Pangani na barabara unganishi zenye urefu wa jumla ya kilometa 25.6, katika sehemu ya Pangani–Tungamaa.
Amesema mradi huo unatekelezwa na mkandarasi Shandong Limited kutoka China kwa gharama ya shilingi bilioni 124.6, chini ya usimamizi wa kampuni ya Lea kutoka India, huku ufadhili ukitolewa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mhandisi Msama ameongeza kwa kusema kuwa, kazi za msingi na nguzo zote tisa za daraja hilo zimekamilika, huku ujenzi wa deck (sehemu ya juu ya daraja ambako magari na watembea kwa miguu hupita) ukiendelea kwa kutumia teknolojia ya Moving Scaffolding System (MSS).
“Ujenzi wa daraja hili kimsingi umetumia teknolojia mpya ndani ya nchi yetu ya Tanzania. Kama mnavyoona, tukiangalia kwenye daraja letu mbele utaona kuna vyuma ambavyo tumeshaviseti pale, ile system nzima ile ndiyo inaitwa Moving Scaffolding System (MSS),” amesema Mhandisi Msama
Vilevile ameeleza kuwa, kukamilika kwa mradi huo kutarahisisha usafiri na usafirishaji wa bidhaa, kupunguza utegemezi wa vivuko, kuongeza fursa za biashara na kuchochea ukuaji wa sekta ya utalii, hususan kwa wananchi wa Pangani, Tanga na maeneo mengine.
Aidha, ametoa shukrani kwa Serikali ya Awamu ya Sita, Wizara ya Ujenzi na uongozi wa TANROADS kwa ushirikiano na usimamizi unaowezesha mradi huo kutekelezwa.
“Naomba nichukue nafasi hii kuishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Awamu ya Sita ambayo inaongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa sababu bila yeye huu mradi usingewezekana,” amesema Mhandisi Msama