News

KASEKENYA ATAKA BARABARA ZA AFCON ARUSHA KUKAMILIKA IFIKAPO DISEMBA

Naibu Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya ameutaka Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), kuhakikisha inamsimamia vizuri mkandarasi anaejenga barabara ya Kona ya Nairobi-Kisongo na Kona ya Nairobi-Soko la Kilombero ili ikamilike ifikapo Disemba mwaka huu.

Akizungumza alipokagua ujenzi wa barabara hiyo Eng. Kasekenya amehimiza umuhimu wa ushirikiano baina ya taasisi za umma ili kufikia lengo Serikali.

" AFCON ni fursa muhimu kwa taifa hivyo barabara hizi zikikamilika kwa ubora licha ya kurahisisha usafiri wakati wa michuano hii pia itaongeza mtandao wa barabara jijini Arusha na kuchochea fursa za kiuchumi", amesisitiza Eng. Kasekenya.

"Maelekezo ya Mheshimiwa Rais ni kwamba hii miradi isikwame, ikamilike ndani ya muda na kwa upande wetu ndani ya muda ni Disemba mwaka huu," amesisitiza Naibu Waziri Kasekenya.

Ujenzi wa barabara hizo pia unajumuisha njia  za watembea kwa miguu, taa za barabarani ili kuufanya mji wa Arusha kuwa wa kisasa na wa kuvutia.

"AFCON ni ya muda mfupi, lakini miundombinu  itaendelea kubaki na kwa muda mrefu, " ameongeza Eng. Kasekenya.

Naibu Waziri huyo wa Ujenzi amezitaka taasisi zinazohusika na huduma za maji, umeme, na mawasiliano kushirikiana kwa karibu na wakandarasi ili kuhamisha haraka miundombinu ya chini ya ardhi (mabomba na nyaya) katika  maeneo ya ujenzi ili kuendana na kasi ya mkandarasi.

Meneja wa TANROADS mkoa wa Arusha Eng. Reginald Masawe amemhakikishia Naibu Waziri Kasekenya kuwa watahakikisha ujenzi huo unakamilika kwa wakati ambapo kwa sasa ujenzi unaendelea kwa usiku na mchanga ili kuhakikisha unatoa fursa kwa wananchi kunufaika na barabara hizo kiuchumi na kijamii.

Huku akielezea kwa jumla ya kiasi cha fedha bilioni 10.2 zimelipwa kama fidia kwa wananchi 48 waliopisha mradi huo.