News

UJENZI WA DARAJA LA KISA WAFUFUA SHUGHULI ZA KIUCHUMI, WANANCHI WASEMA USAFIRI SASA NI USIKU NA MCHANA

Ujenzi wa Daraja la Kisa umefungua fursa mpya za kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa maeneo ya bonde, huku shughuli za biashara na usafirishaji zikiendelea kwa urahisi zaidi baada ya kuondolewa kwa changamoto za usafiri zilizodumu kwa muda mrefu.

Akizungumza kuhusu manufaa ya daraja hilo, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Talanda mkoani Rukwa Oscar Jacob amesema, ujenzi wake umewezesha wafanyabiashara na wasafirishaji kufanya shughuli zao wakati wote, ikiwemo kusafirisha samaki na mazao pamoja na kuwahisha wagonjwa hospitalini.

"Sasa hivi biashara hazilali, bodaboda wanasafirisha usiku na mchana samaki, magari yanapita vizuri, wagonjwa wanapita vizuri... Kiukweli historia ya hili daraja imekuja kuwa ni future mpya kwenye maisha ya wana-bonde na kututengenezea dira mpya kwa maisha ya kwenye bonde," amesema Jacob.

Amesema hali hiyo imeleta matumaini mapya kwa wananchi wa bonde, ambao sasa wanaweza kufika maeneo mbalimbali kwa urahisi zaidi na kuendesha shughuli zao bila kuathiriwa na changamoto za usafiri zilizokuwapo awali.

Hata hivyo, Jacob ameiomba Serikali kuendelea na jitihada za kuboresha miundombinu katika maeneo mengine korofi ya ukanda huo, akitaja Mto Wisa na Kijiji cha Sakalilo kuwa miongoni mwa maeneo yanayohitaji hatua zaidi.

Kwa upande wake, mkazi wa eneo hilo Boniface Edward amesema, kukamilika kwa Daraja la Kisa kumekuwa na mabadiliko makubwa katika maisha ya wananchi, hususan katika usafirishaji wa mazao, samaki na wagonjwa, ambao sasa wanaweza kusafirishwa kwa urahisi zaidi wakati wa mchana na usiku.

Amesema uwepo wa daraja hilo umeongeza ufanisi wa shughuli za kiuchumi na kupunguza vikwazo vya usafiri vilivyokuwa vikikabili wananchi wa eneo hilo.