News

KASEKESE–IKOLA–KALEMA: UJENZI WAFIKIA ASILIMIA 45

Ujenzi wa barabara ya Kasekese–Ikola–Kalema yenye urefu wa kilomita 56.1 umefikia asilimia 45, huku kazi za ujenzi zikiendelea katika maeneo mbalimbali ya mradi huo, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuboresha usafirishaji na kuchochea shughuli za kiuchumi katika Mkoa wa Katavi.

Akizungumza wakati wa kutoa taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo, Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Katavi, Mhandisi Martin Mwakabende, amesema hadi sasa baadhi ya tabaka za barabara zimekamilika na zipo tayari kwa ajili ya kuwekwa lami.

Amesema TANROADS inaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo, huku matarajio yakiwa ni kukamilisha ujenzi wa tabaka la kiwango cha lami kwa urefu wa kilomita 26 ifikapo Oktoba mwaka huu.

Ameeleza kuwa mradi huo unatarajiwa kukamilika ifikapo Oktoba 2027 na kuanza kutumika, hatua ambayo itakuwa na mchango mkubwa katika kurahisisha usafirishaji wa watu na mizigo kuelekea Bandari ya Kalema.

Kwa upande wake, Mhandisi Mshauri kutoka kampuni ya Intercontinental amesema barabara hiyo ina umuhimu mkubwa kimkakati kwa kuwa inaunganisha Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kupitia Bandari ya Kalema.

Amesema kukamilika kwa barabara hiyo kutarahisisha usafirishaji wa bidhaa, kuongeza fursa za biashara na kuchochea shughuli za kiuchumi kwa wananchi wanaoishi katika maeneo yanayopitiwa na mradi huo.

Aidha, amesema mradi huo tayari umeanza kuleta manufaa kwa jamii kupitia ajira na fursa mbalimbali, ambapo zaidi ya wananchi 300 wamenufaika kwa kupata ajira katika shughuli zinazohusiana na utekelezaji wa mradi.

Kwa wananchi wa maeneo yanayopitiwa na barabara hiyo, kukamilika kwake kunatarajiwa kuwa kichocheo cha maendeleo kwa kurahisisha usafirishaji wa mazao na bidhaa, kuongeza mwingiliano wa kibiashara na kuboresha upatikanaji wa huduma mbalimbali.

Mhandisi Mwakabende amesisitiza kuwa TANROADS itaendelea kushirikiana kwa karibu na mkandarasi pamoja na Mhandisi Mshauri kuhakikisha kazi zinafanyika kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa na mradi unakamilika ndani ya muda uliopangwa.